Israel yazuia meli ya misaada iliyokuwa ikielekea Gaza kwenye bahari ya kimataifa, yakamata 12

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 11, 2025

Meli iliyoripotiwa kubeba mizigo ya misaada ya kibinadamu ikiwasili kwenye bahari karibu na bandari ya Ashdod, kusini mwa Israel, tarehe 9 Juni 2025. (Picha na Jamal Awad/Xinhua)

Meli iliyoripotiwa kubeba mizigo ya misaada ya kibinadamu ikiwasili kwenye bahari karibu na bandari ya Ashdod, kusini mwa Israel, tarehe 9 Juni 2025. (Picha na Jamal Awad/Xinhua)

JERUSALEM - Israel imesema kuwa imeikamata Meli Madleen, chombo kilichokuwa kimebeba wanaharakati 12 kilichokuwa kikijaribu kuvunja kizuizi chake cha majini kwenye Ukanda wa Gaza na kuisindikiza hadi kwenye bandari ya Ashdodi, ambapo meli hiyo ilifika kwenye bandari hiyo kubwa zaidi nchini Israel, baada ya kukamatwa na vikosi vya Israel kwenye bahari ya kimataifa mapema Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imesema.

"Wanaharakati hao, akiwemo mwanaharakati wa tabianchi wa Sweden Greta Thunberg na mtetezi wa haki za binadamu wa Brazil Thiago Avila, wanafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na watafukuzwa nchini," wizara hiyo imesema.

"Yati imetia nanga kwenye Bandari ya Ashdod muda mfupi uliopita," wizara hiyo imeandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, ikiongeza kuwa abiria walikuwa na afya njema, ambapo picha zilizotolewa na wizara hiyo zinawaonyesha Thunberg na Avila wakionekana kuchoka lakini bila kujeruhiwa.

Adalah, shirika la kutetea haki za kisheria lenye makao yake makuu nchini Israel linalowawakilisha wanaharakati hao, limesema mawasiliano na kundi hilo yalipotea muda mfupi baada ya meli hiyo kuzuiliwa majira ya saa 9:00 alasiri kwa saa za Israel. "Tangu wakati huo, mawasiliano na wanaharakati yalipotea," limesema katika taarifa.

Muungano wa Freedom Flotilla, ambao uliandaa safari hiyo, umeishutumu Israel kwa kinyume cha sheria, ukisema meli hiyo "ilitekwa nyara" kwenye bahari ya kimataifa. Kundi hilo limesema abiria walikabiliwa na shinikizo la kisaikolojia, ikiwemo matumizi ya vinyunyizi vyeupe vya kuwasha, kukwama kwa mawasiliano, na usambazaji wa kelele sumbufu kupitia redio.

Chombo hicho kiliripotiwa kubeba mizigo ya misaada ya kibinadamu, ikiwemo chakula na vifaa vya matibabu, iliyokusudiwa kuelekea Gaza.

Tukio hilo la Jumatatu linakuja mwezi takriban mmoja baada ya chombo kingine Conscience, kuharibiwa katika shambulizi linalodaiwa kuwa la droni kwenye bahari ya kimataifa karibu na Malta.

Israel iliweka vizuizi vya vyombo vya majini katika eneo la Gaza mwaka 2007 baada ya Hamas kuchukua udhibiti wa eneo hilo. Vizuizi hivyo viliimarishwa zaidi kufuatia shambulizi baya la Hamas kuvuka mpaka kusini mwa Israel Oktoba 2023.

Vita hivyo, sasa katika mwezi wa 21, vimeharibu miundombinu ya Gaza na kuwafanya wakaazi wake milioni 2.3 wako katika janga kali la kibinadamu. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya juu ya njaa kali inayokuja, huku watu wote wakikabiliwa na ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha