LEGOLAND Shanghai Resort kuanza shughuli za majaribio kabla ya kufunguliwa Julai

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 27, 2025
LEGOLAND Shanghai Resort kuanza shughuli za majaribio kabla ya kufunguliwa Julai
Picha hii iliyopigwa tarehe 26 Mei 2025 ikionyesha miundo ya LEGO katika eneo la LEGOLAND Shanghai resort mjini Shanghai, mashariki mwa China. (Xinhua/Chen Aiping)

SHANGHAI - LEGOLAND Shanghai Resort, LEGOLAND kubwa zaidi duniani, imetangaza jana Jumatatu kuwa itazindua uendeshaji wa majaribio kuanzia Jumamosi wiki hii ikiwa ni sehemu ya awamu yake ya mwisho ya kabla ya ufunguzi ambapo wageni maalum wataalikwa kufurahia bustani hiyo ya mapumziko na kusaidia kuweka kila kitu katika hali ya utayari kabla ya ufunguzi rasmi tarehe 5 Julai mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waendeshaji, vivutio, mikahawa, maonyesho na vyumba vya hoteli vitajaribiwa ili kuhakikisha sifa ya viwango vya juu, uvumbuzi na burudani.

Wameeleza kuwa, eneo hilo la mapumziko litafunguliwa kwa sehemu mbalimbali katika kipindi hiki -- kukusanya mrejesho wa maoni na kufanya marekebisho ya mwisho ili kuhakikisha huduma bora zaidi kwa wageni.

Likiwa linapatikana katika Wilaya ya Jinshan ya Shanghai, eneo hilo la mapumziko lenye ukubwa wa mita za mraba 318,000 ni bustani ya mandhari ya LEGO na kivutio cha hoteli kwa watoto wa miaka 2 hadi 12 na familia zao. Eneo hilo la mapumziko lina zaidi ya vifaa 75 za michezo, maonyesho na vivutio, vilevile maelfu ya miundo ya LEGO katika eneo nane la bustani hiyo.

Mji wa Shanghai mashariki mwa China unakuwa kivutio kikuu cha uwekezaji kwa waendeshaji bustani za mandhari za kimataifa, wakati ambapo wanatafuta kunufaika na masoko yanayopanuka ya burudani na utalii ya China. Kuanzishwa kwa LEGOLAND Shanghai Resort kunafuatia mafanikio yaliyopatikana na Shanghai Disney Resort.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha