Rais wa Afrika Kusini apanga kufanya mazungumzo na viongozi wa G7

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 11, 2025

JOHANNESBURG - Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kwamba anapanga kufanya mikutano ya pande mbili na viongozi kadhaa wa Kundi la Nchi Saba (G7), akiwemo Rais Donald Trump wa Marekani, wakati wa mkutano ujao wa G7.

"Ninatumai kwamba tutakapokutana na viongozi wengine wa nchi mbalimbali ya G7, tutakuwa na uwezo wa kuzungumza nao ipasavyo. Nitakuwa na mikutano ya pande mbili na Chansela wa Ujerumani, na Waziri Mkuu wa Canada, na bila shaka, pia nitakuwa nikikutana na Rais Trump, ambaye tulikutana kwenye Ikulu ya White House," amesema jana Jumanne.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Pretoria, Ramaphosa kwa mara nyingine tena ameielezea ziara yake ya hivi karibuni katika Ikulu ya White House kuwa ya mafanikio, licha ya ukosoaji unaozunguka madai yasiyo na msingi ya "mauaji ya kimbari dhidi ya weupe".

Amesema kuwa malengo makuu ya ziara hiyo ilikuwa kurekebisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kufuatilia masuala ya kibiashara.

"Ni muhimu kwetu kujiweka kwenye nafasi mpya katika muundo wa siasa za kijiografia wenye misukosuko," amesema.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na ushuru wa biashara wa Marekani. Ramaphosa amewaambia waandishi wa habari kuwa majadiliano kuhusu biashara yanaendelea, na "mazungumzo hayo yanafanyika."

Ramaphosa amesema amealikwa na Canada na kwamba mkutano wa G7 ni fursa nzuri kwa Afrika Kusini "kueneza" ujumbe wake wa G20 "na namna tunavyotaka kuona matokeo mazuri kutoka G20."

"Tutakwenda kuutumia (mkutano wa G7) kama jukwaa la kuanza kuimarisha kile tunachotaka kufikia mwezi Novemba wakati Mkutano wa Kilele wa (G20) utakapofanyika hapa, hivyo ni fursa kubwa na tunatumai kuwa kutakuwa na matokeo mazuri kutoka kwake," Ramaphosa amesema. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha