Wang Yi atoa wito wa mafanikio mengi zaidi katika ushirikiano kati ya China na Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 13, 2025

CHANGSHA - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi ametoa wito wa kuwepo simulizi nyingi zaidi za mafanikio kutokana na ushirikiano kati ya China na Afrika ili kutoa mchango kwa ajili ya urafiki kati ya China na Afrika, na kuleta matumaini kwa maendeleo ya kujitegemea na maisha bora kwa watu wa Bara la Afrika.

Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ametoa mfano wa mkulima na mjasiriamali wa Gambia Musa Darboe, ambaye amefaidika sana na teknolojia ya mpunga chotara ya China.

Wang ameyasema Jumatano wakati akizungumza na Darboe kwenye tafrija ya kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika mjini Changsha, mji mkuu wa Mkoa wa Hunan, katikati mwa China.

Kwenye tafrija hiyo, Darboe alielezea simulizi yake ya namna ya kutumia teknolojia hiyo ya mpunga chotara ya mwanasayansi wa China Yuan Longping na kuongeza kwa kiasi kikubwa mavuno yake ya mpunga, akisema kwamba kwa msaada wa wataalam wa kilimo wa China barani Afrika, amepata maisha mazuri, na watu wa maskani yake wameiaga njaa.

Darboe, ambaye ameleta mpunga wake kutoka Gambia hadi China kama ishara ya kumuenzi Yuan, ameelezea nia yake ya kujifunza zaidi kuhusu teknolojia za kilimo na uzoefu wa China katika mambo ya kisasa, na kuhimiza ushirikiano wa kina, mpana zaidi kati ya nchi hizo mbili.

“Kipaumbele muhimu cha uhusiano wa kirafiki kati ya China na nchi za Afrika ni kuboresha maisha ya Waafrika wa kawaida” Wang amesema, akiongeza kwamba China itaendelea kufuata mtazamo sahihi wa maslahi ya pamoja, na kutoa manufaa zaidi halisi kwa watu wa bara la Afrika.

Hunan ni maskani kwa Yuan Longping, mwanasayansi wa mpunga ambaye alitoa mchango mkubwa katika uundaji spishi za mpunga nchini China na anajulikana kama "baba wa mpunga chotara." Yuan aliaga dunia mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 91.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha