Israel yafanya mashambulizi dhidi ya Iran, ikimuua kamanda mkuu wa IRGC

(CRI Online) Juni 13, 2025

(Picha/CFP)

(Picha/CFP)

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema, nchi hiyo imefanya "mashambulizi ya kuzuia" dhidi ya Iran, ambapo Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limethibitisha katika taarifa yake mapema leo Ijumaa kwamba ndege zake za kivita zimekamilisha mashambulizi ya hatua ya kwanza, hasa kupiga maeneo kadhaa lengwa ya kijeshi, vikiwemo vituo vya nyuklia katika maeneo tofauti ya Iran.

Kwa mujibu wa habari iliyotolewa na shirika rasmi la habari la Iran, IRNA Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) Hossein Salami na Gholam-Ali Rashid, kamanda wa Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya ya Iran, wameuawa katika mashambulizi hayo ya anga.

Mashambulizi hayo ya anga ya Israel pia yameua wanasayansi wawili wa nyuklia wa Iran, waliotambuliwa kwa majina ya Mohammad-Mehdi Tehranchi na Fereydoun Abbasi, ripoti hiyo ilisema.

Kituo cha televisheni cha Iran, IRIB pia kimeripoti kuwa, milipuko mikubwa imesikika katika maeneo ya mji mkuu wa nchi hiyo, Tehran mapema jana, na chanzo chake bado hakijafahamika.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema katika hotuba yake kwa njia ya video kwamba lengo la operesheni hiyo inayoendelea ni "kupiga miundombinu ya nyuklia ya Iran, viwanda vya makombora ya balestiki vya Iran, na uwezo wa kijeshi wa Iran," na itaendelea "kwa siku nyingi kadri iwezekanavyo."

Akizungumzia mashambulizi hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema kuwa Marekani hajatoa uungaji mkono wowote na haihusiki katika mashambulizi hayo na kwamba Israel imefanya maamuzi hayo kwa maamuzi ya upande mmoja.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha