Kenya yapitisha bajeti ya dola bilioni 32.5 kwa mwaka wa fedha 2025/26

(CRI Online) Juni 13, 2025

Serikali ya Kenya imewasilisha bajeti ya shilingi trilioni 4.2 (sawa na dola bilioni 32.5 za Marekani) kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026, ikiwa na mapendekezo yanayolenga kuchochea shughuli za kiuchumi.

Waziri wa fedha na mipango ya uchumi wa Kenya Bw. John Mbadi, amewasilisha taarifa ya bajeti mbele ya Bunge la Taifa jana Alhamisi, akisema kuwa serikali inataka kuhimiza ukuaji endelevu wa uchumi ili kuboresha maisha ya watu, kuchochea biashara na ustawi wa viwanda.

Bw. Mbadi amesema mwaka 2024, uchumi wa Kenya ulikua kwa asilimia 4.7, ukichochewa na ukuaji chanya katika sekta zote isipokuwa ujenzi na madini, kiwango ambacho ni cha chini ikilinganishwa na asilimia 5.7 ya mwaka 2023, hasa kutokana na athari za mafuriko katika robo ya pili na maandamano ya kupinga sheria ya fedha katika robo ya tatu ya mwaka 2024.

Licha ya kudorora huko Bw. Mbadi amesema uchumi wa Kenya unaendelea kuwa himilivu, ukirekodi kiwango cha wastani cha ukuaji wa asilimia 5.2 kwa mwaka 2023 na 2024, ukipita ukuaji wa kimataifa wa asilimia 3.3, na ule wa eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara wa asilimia 3.8.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha