Ikulu ya White House yasema Trump kuamua juu ya hatua dhidi ya Iran ndani ya wiki mbili

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 20, 2025

Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Washington, D.C., Marekani, Juni 19, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Washington, D.C., Marekani, Juni 19, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

NEW YORK - Rais Donald Trump wa Marekani atafanya uamuzi kama ataamuru mashambulizi dhidi ya Iran ndani ya wiki mbili, Msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari jana Alhamisi.

"Kutokana na uwezekano mkubwa wa kufanya mazungumzo na Iran katika siku za karibuni, nitafanya uamuzi wangu ndani ya wiki mbili zijazo," Leavitt amesoma taarifa kutoka kwa Trump ambaye alijibu uvumi kuhusu Marekani itahusika moja kwa moja katika mgogoro kati ya Iran na Israel.

Leavitt amesema Iran lazima ikubali kutorutubisha uranium, na lazima isiwe na uwezo wa kupata silaha ya nyuklia kama sehemu ya makubaliano yoyote ya kidiplomasia.

Mawasiliano kati ya Marekani na Iran "yameendelea" huku pande hizo mbili zikishiriki mazungumzo, Leavitt amesema, akirejelea ripoti za mapema siku hiyo ya Alhamisi kwamba mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi walikuwa wamezungumza kwa njia ya simu mara kadhaa tangu Israel ilipoanza mashambulizi yake dhidi ya Iran Juni 13, katika jitihada za kutatua mgogoro huo kwa njia ya kidiplomasia.

Mazungumzo hayo yanajadali kwa ufupi pendekezo la Marekani kwa Iran linalolenga kuunda shirika la kikanda ambalo litarutubisha madini ya uranium nje ya Iran, jambo ambalo hadi sasa Tehran imelikataa, vyombo vya habari vya Marekani vimenukuu wanadiplomasia watatu wakisema kwa sharti la kutotajwa majina yao.

Araghchi amemwambia Witkoff kwamba Tehran "inaweza kuonyesha unyumbufu wake katika suala la nyuklia" kama serikali ya Marekani itaishinikiza Israel kumaliza vita, akiongeza kuwa Tehran haitarejea kwenye mazungumzo isipokuwa pale tu Israel itakaposimamisha mashambulizi, vyombo vya habari vya Iran vimemnukuu mwanadiplomasia wa eneo hilo.

Trump aliidhinisha mipango ya mashambulizi dhidi ya Iran Jumanne usiku wiki hii, lakini akasita kutoa uamuzi wa mwisho kama ikitokea Iran kukubali kuachana na mpango wake wa nyuklia, vyombo vya habari viliripoti.

Trump amekuwa akikutana na timu yake ya usalama ya taifa kwenye Chumba cha Hali kila siku tangu siku hiyo ya Jumanne.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha