Tanzania mwenyeji mkutano wa mabaraza ya vyombo vya habari Afrika

(CRI Online) Juni 23, 2025

Wakati jitihada mbalimbali za kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania zikiendelea kufanyika, nchi hiyo itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa mabaraza ya vyombo vya habari barani Afrika uliopangwa kufanyika Julai 14 hadi 17, 2025 jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Baraza la Vyombo vya Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura amesema mbali na mkutano huo, MCT pia iko mbioni kufanya utafiti kuangazia mabadiliko ya sheria na uwepo wa bodi ya ithibati, maana na athari zake katika tasnia ya habari.

Sungura amesema baraza hilo linaandaa mkutano huo kwa mara ya kwanza kwa kushirikiana na Mtandao wa Mabaraza Huru ya Vyombo vya Habari Afrika, Umoja wa Mabaraza ya Vyombo vya Habari ya Afrika Mashariki na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Tanzania kama mshirika mahsusi.

Kwa mujibu wa takwimu za Kielezo cha Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (World Press Freedom Index) kinachoratibiwa na Taasisi ya Reporters Without Borders (RWB) Tanzania sasa inashika nafasi ya 97 katika nchi zinazozingatia uhuru wa vyombo vya habari ikiwa imepanda kutoka nafasi ya 142 mwaka 2023.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha