Tanzania yawarejesha raia wake 147 kutoka Israel na Iran

(CRI Online) Juni 24, 2025

Serikali ya Tanzania imewarejesha nyumbani raia wake 147 kati ya 663 waliokuwa wakiishi Israel na Iran wakati hali ya usalama ikiendelea kuwa mbaya katika eneo la Mashariki ya Kati.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa nchini Tanzania, Dennis Londo ametoa taarifa hiyo bungeni mjini Dodoma, alipokuwa akijibu maoni ya wabunge wakati wa mjadala unaoendelea wa bajeti ya taifa na mpango wa maendeleo kwa mwaka 2025/2026.

Wakati huohuo, Uganda imelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran, ikiyaeleza kuwa ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa, na kutaka kusimamishwa mara moja kwa mapigano hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Jeje Odongo amesema hayo alipokuwa akihudhuria kikao cha 51 cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Mataifa ya Kiislamu (OIC) kilichofanyika nchini Uturuki mwishoni mwa wiki iliyopita.

Odongo pia amelaani mashambulizi yanayoendelea dhidi ya Wapalestina, hususan katika Ukanda wa Gaza, ambayo yamesababisha vifo vya raia wengi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha