

Lugha Nyingine
Colombia na Uzbekistan zajiunga na Benki ya BRICS
Dilma Rousseff, Rais wa zamani wa Brazili na Rais wa Benki ya Maendeleo Mapya (NDB), akizungumza kwenye Mkutano wa 10 wa Mwaka wa NDB mjini Rio De Janeiro, Brazil, Julai 4, 2025. (Picha na Claudia Martini/Xinhua)
RIO DE JANEIRO - Colombia na Uzbekistan zimejiunga rasmi na Benki ya Maendeleo Mapya (NDB), zikipanua idadi ya nchi wanachama wa benki hiyo mkopeshaji wa kimataifa inayojulikana pia kwa jina la Benki ya BRICS, Rais wa taasisi hiyo, Dilma Rousseff, ametangaza mjini Rio De Janeiro, Brazil Jumamosi.
Tangazo hilo limekuja kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mkutano wa 10 wa Bodi ya Wakurugenzi ya NDB, kabla ya Mkutano wa Kilele wa 17 wa BRICS ulioanza jana Jumapili na utaendelea leo Jumatatu.
Rais huyo amesema, Bodi ya Magavana wa benki hiyo imeidhinisha kujiunga kwa nchi hizo mbili, ikifanya idadi ya jumla ya nchi wanachama wake kufikia 11.
Nchi wanachama wa sasa ni pamoja na Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini, Bangladesh, Falme za Kiarabu, Misri, Algeria, Colombia na Uzbekistan.
"Tuna nchi nyingine kadhaa zilizo chini ya ukaguzi na kuhakikishwa, na zinaweza kujiunga na benki hiyo katika siku zijazo," amesema Rousseff, akiongeza kuwa mazungumzo yanabaki kuwa siri kulingana na uamuzi wa bodi.
Akisema kuwa dhamira ya benki hiyo ni kuhudumia Nchi za Kusini, amesema NDB inalenga kufadhili uvumbuzi, sayansi na teknolojia ili kuzisaidia nchi za BRICS kukidhi matakwa ya Mapinduzi ya Nne ya Kiviwanda.
Akisisitiza kuwa NDB inaheshimu mamlaka na vipaumbele vya maendeleo vya nchi wanachama, na hashinikizi miradi au masharti ya mikopo, Rousseff amesema: "Moja ya tofauti zetu kuu ni kwamba nchi wanachama wote ni sawa, na kila sauti inasikika.”
“Benki hii ni taasisi ya karne ya 21 inayozingatia mshikamano, usawa na heshima kwa mamlaka ya kitaifa,” ameongeza.
Ikiwa ilianzishwa mwaka 2015 na Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini NDB ni benki ya maendeleo ya pande nyingi yenye lengo la kukusanya rasilimali kwa ajili ya miradi ya miundombinu na maendeleo endelevu katika BRICS na nchi nyingine zenye uchumi wa masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea.
Ikiwa na makao yake makuu mjini Shanghai, China NDB imeshaidhinisha miradi zaidi ya 120 ya uwekezaji yenye thamani ya jumla ya dola bilioni 40 za Marekani na inahusisha maeneo kadhaa muhimu, yakiwemo nishati safi na ufanisi wa nishati, miundombinu ya usafiri, ulinzi wa mazingira, usambazaji maji na usafi wa mazingira, miundombinu ya kijamii na miundombinu ya kidijitali.
Dilma Rousseff, Rais wa zamani wa Brazili na Rais wa Benki ya Maendeleo Mapya (NDB), akizungumza kwenye Mkutano wa 10 wa Mwaka wa NDB mjini Rio De Janeiro, Brazili, Julai 4, 2025. (Picha na Claudia Martini/Xinhua)
Dilma Rousseff, Rais wa zamani wa Brazili na Rais wa Benki ya Maendeleo Mapya (NDB), akizungumza kwenye Mkutano wa 10 wa Mwaka wa NDB mjini Rio De Janeiro, Brazili, Julai 4, 2025. (Picha na Claudia Martini/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma