

Lugha Nyingine
Rais Museveni wa Uganda ateuliwa kuwa mgombea urais wa chama tawala katika uchaguzi wa 2026
Rais wa Uganda Yoweri Museveni (Kulia) na mkewe wakiwapungia mkono wafuasi baada ya uteuzi mjini Kampala, Uganda, Julai 5, 2025. (Picha na Nicholas Kajoba/Xinhua)
KAMPALA - Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameteuliwa kuwa mgombea pekee wa kukiwakilisha chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) katika uchaguzi wa urais mwaka ujao ambapo Museveni, ambaye atawania awamu ya saba ya miaka mitano, amependekezwa na NRM kwenye mkutano uliofanyika katika mji mkuu, Kampala juzi Jumamosi.
Uteuzi wake bila kupingwa unamaanisha kuwa chama hakitafanya uchaguzi wa mchujo ili kumchagua mpeperusha bendera wa urais.
Tom Buttime, mwanahistoria wa NRM na waziri wa utalii, wanyamapori na mambo ya kale wa Uganda, ambaye alimteua rasmi Museveni, amemsifu rais huyo kwa kudumisha utulivu wa nchi.
"Uchumi unaimarika huku kukiwa na amani, uhai wa maisha na uhuru nchini," Buttime amesema.
Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi wake, Museveni, mwenye umri wa miaka 80, amesema kuwa iwapo atachaguliwa tena, atayapa kipaumbele maeneo sita muhimu: amani, maendeleo, uletaji wa utajiri, ajira, huduma na masoko.
Pia ameelezea nia yake ya kuiinua Uganda kutoka nchi yenye uchumi wa mapato ya chini-kati hadi hadhi ya mapato ya juu-kati ifikapo mwaka 2040.
"Niko tayari kutoa mchango wangu katika miaka mitano ijayo nikiwa kama mwenyekiti wa NRM na rais," amesema Museveni.
Uganda imepanga kufanya uchaguzi mkuu Januari 2026, huku wagombea kadhaa wa upinzani wakitarajiwa kujiunga na kinyang'anyiro hicho.
Watu wakisubiri matokeo ya uteuzi mjini Kampala, Uganda, Julai 5, 2025. (Picha na Nicholas Kajoba/Xinhua)
Rais wa Uganda Yoweri Museveni (katikati, mbele) na mkewe wakiwa katika picha ya kundi na wanachama wa chama chake baada ya uteuzi mjini Kampala, Uganda, Julai 5, 2025. (Picha na Nicholas Kajoba/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma