Trump atangaza kutoza ushuru wa asilimia 25 hadi 40 kwa nchi 14

(CRI Online) Julai 08, 2025

Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kuwa nchi hiyo itatoza ushuru wa asilimia 25 hadi 40 kwa bidhaa kutoka nchi 14 ikiwemo Afrika Kusini kuanzia tarehe mosi, Agosti.

Kwa mujibu wa barua alizowaandikia viongozi wa nchi hizo 14 zilizochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa "Truth Social", Rais Trump amesema Japan, Korea Kusini, Malaysia, Tunisia na Kazakhstan zitatozwa ushuru wa 25% mtawalia, Afrika Kusini, Bosnia na Herzegovina zitatozwa ushuru wa 30%, Indonesia itatozwa ushuru wa 32%, Serbia na Bangladesh ushuru wa 35%, Thailand na Cambodia ushuru wa 36%, huku Laos na Myanmar zikikabiliwa na ushuru wa hadi 40%.

Katika barua hizo zenye maudhui yanayofanana, Trump ametahadharisha viongozi wa nchi hizo kwamba kama wakitaka kujibu kwa kuongeza ushuru, Marekani itaongeza zaidi ushuru kwa kiasi kinacholingana juu ya kiwango cha sasa. Wakati huo huo, ameeleza kuwa, kama nchi hizo au kampuni zao zitaamua kuzalisha bidhaa nchini Marekani, hazitatozwa ushuru huo.

Amesema kuwa, iwapo nchi hizo zitafungua masoko yao ya ndani kwa Marekani na vilevile kuondoa ushuru na vikwazo visivyo vya kiushuru, basi Marekani itafikiria kurekebisha kiwango cha ushuru kilichotajwa kwenye barua, jambo ambalo pia litaamuliwa na uhusiano kati ya Marekani na nchi husika.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha