

Lugha Nyingine
Jinsi Kiswahili inavyojenga daraja la utamaduni kati ya China na Tanzania
Zhang Xiaozhen, mkurugenzi wa China wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akihojiwa jijini Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 4 Julai 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)
DAR ES SALAAM - Asubuhi tulivu, ndani ya darasa lenye mwanga wa jua katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nchini Tanzania, kundi la walimu wa lugha ya Kichina walikuwa wakikariri salamu za lugha ya Kiswahili.
"Habari za asubuhi," mmoja alisema, akitabasamu. "Nzuri sana," mwingine alijibu. Majibizano haya rahisi, "habari za asubuhi" na "nzuri sana," ni zaidi ya somo la lugha tu. Inawakilisha harakati inayokua ya shauku ya kiutamaduni, kuheshimiana na mawasiliano ya kielimu kati ya China na Tanzania.
Wakati jumuiya ya kimataifa ikiadhimisha Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani jana Jumatatu, Julai 7, moyo wa siku hii unaonekana dhahiri katika Taasisi ya Confucius ya chuo kikuu kikubwa zaidi nchini Tanzania, ambapo raia wa China walikuwa wakikikumbatia Kiswahili si tu kama lugha bali kama lango la kuelewa maisha ya wenyeji.
Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), katika kikao chake cha 41 kilichofanyika Paris, Ufaransa, mwaka 2021, uliitangaza Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, ikikifanya kiwe lugha ya kwanza ya Afrika kutambuliwa kwa namna hiyo na Umoja wa Mataifa.
Yang Xin, mwalimu wa lugha ya Kichina katika Taasisi hiyo ya Confucius, amesema kujifunza Kiswahili kumekuwa vyote changamoto na hitaji.
"Mwanzoni, sikuweza kuelewa chochote," amekumbushia. "Lakini shukrani kwa Taasisi ya Confucius, nilianza kujifunza. Inanisaidia kubadilika kuendana na maisha ya hapa na kuunganishwa na watu” ameeleza.
Athari za ufasaha wa lugha ya Kiswahili huenda zaidi ya darasani.
Kwa mujibu wa Emmanuel Legonga, mwalimu mwenyeji Mtanzania wa lugha ya Kichina katika Taasisi ya Confucius, ambaye pia anafundisha Kiswahili kwa Wachina wanaoishi nchini Tanzania, kuzungumza lugha ya kienyeji kuna athari za matunda katika tasnia mbalimbali.
"Kwenye miradi ya miundombinu kama vile reli na bandari, wakati mameneja au wahandisi wa China wanapotumia Kiswahili, inajenga imani kwa wafanyakazi wenyeji," Legonga ameelezea. "Inaondoa hisia ya umbali. Wafanyakazi wanahisi kuzingatiwa na kuheshimiwa."
Legonga alikuwa na furaha aliposema kwamba mmoja wa wanafunzi wake wa Kiswahili ni Zhang Xiaozhen, mkurugenzi wa China wa Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa maoni ya Zhang, shauku ya Kiswahili miongoni mwa raia wa China inazidi kuongezeka.
"Kwenye darasa letu lililopita, Wachina zaidi ya 70 walijiunga na masomo ya Kiswahili. Mwaka huu, karibu 90 wamedahiliwa," amesema. "Wengine huanza kujifunza wakiwa China, wengine baada ya kufika. Walimu wa Kichina wapatao 20 wamesoma Kiswahili."
Wakati Mussa Hans, Mkurugenzi wa Tanzania wa Taasisi ya Confucius, alipokuwa akijiandaa kuadhimisha Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani mwaka huu, ametafakari juu ya dhamira pana zaidi ya taasisi hiyo.
"Hatufundishi tu lugha; tunajenga uhusiano. Tunaeneza zote lugha za Kichina na Kiswahili ili watu wetu waweze kuelewana vyema."amesema.
Wanafunzi Wachina wakihudhuria darasa la lugha ya Kiswahili katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jijini Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 4 Julai 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)
Emmanuel Legonga (wa pili, kulia), mwalimu Mtanzania wa lugha ya Kichina katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akiwasaidia wanafunzi Wachina kusoma Kiswahili jijini Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 4 Julai 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)
Mussa Hans, mkurugenzi wa Tanzania wa Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akihojiwa jijini Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 4 Julai 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma