

Lugha Nyingine
Ujerumani yaimarisha uhusiano na eneo la Baltic kwa dhamira imara za kiusalama wakati wa ziara ya rais
Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani (wa pili kushoto, mbele) na Rais Edgars Rinkevics wa Latvia (wa tatu kushoto, mbele) wakitembelea meli ya kivita ya Kikosi cha Majini cha Jeshi la Ujerumani kinachoshiriki kwenye operesheni ya "Baltic Sentry" ya NATO katika Bahari ya Baltic mjini Riga, Latvia, Julai 8, 2025. (Picha na Edijs Palens/Xinhua)
RIGA - Ziara ya siku tatu ya Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani nchini Lithuania na Latvia imesisitiza uungaji mkono mkubwa wa nchi za Ulaya kwa eneo la Baltic, hasa katika ushirikiano wa kiusalama, Steinmeier amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati akihitimisha ziara yake nchini Latvia jana Jumanne, kufuatia ziara yake nchini Lithuania.
Akiwa mjini Riga, mji mkuu wa Latvia, Steinmeier alikutana na Rais Edgars Rinkevics wa Latvia na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Evika Silina ambapo walitembelea meli ya kivita ya Kikosi cha Majini cha Jeshi la Ujerumani kinachoshiriki katika operesheni ya "Baltic Sentry" ya NATO katika Bahari ya Baltic.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya Riga, Steinmeier amelielezea jukumu la Kikosi cha Majini cha Jeshi la Ujerumani katika operesheni hiyo ya Baltic Sentry ya NATO kama mchango mkubwa katika kulinda Bahari ya Baltic na usalama wa miundombinu muhimu chini ya maji.
Kwa upande wake, Rinkevics ameielezea Ujerumani kuwa mshirika wa NATO asiye na mbadala kwa Latvia katika eneo la Bahari ya Baltic, hasa katika kulinda miundombinu muhimu ya chini ya maji, kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari kutoka ofisi ya rais wa Latvia.
Rinkevics pia ameelezea nia ya Latvia katika kuimarisha kwa kina ushirikiano wa kiuchumi na Ujerumani, hasa katika mambo ya ulinzi, ambapo Latvia inatafuta ushirikiano uliopanuliwa.
Awali, wakati wa ziara yake mjini Vilnius, mji mkuu wa Lithuania siku ya Jumapili, Rais Steinmeier aliahidi Ujerumani italinda mamlaka ya Lithuania, akisema: "Usalama wenu ni usalama wetu.”
Ujerumani imeweka rasmi Brigedi ya 45 ya Wanajeshi wa Kivita "Lietuva" nchini Lithuania, ikimaanisha uwekaji wa kwanza wa kudumu wa brigedi kamili ya wanajeshi wa kivita ya Ujerumani nje ya mipaka ya nchi hiyo tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Wakati wa kuzinduliwa kwa brigedi hiyo Mei 22, Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz alisisitiza dhamira ya serikali yake kwa upande wa mashariki wa NATO, akisema uwekaji huo wa brigedi unaonyesha uongozi wa Ujerumani katika ulinzi wa eneo hilo.
Kwa sasa, wanajeshi 500 wa Ujerumani wamewekwa nchini Lithuania, ambapo uwekaji huo kamili, unaojumuisha wanajeshi na wafanyakazi wa kiraia takriban 5,000, na vifaa na vitu muhimu, unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2027.
Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani (kushoto) akipeana mkono na Waziri Mkuu wa Latvia Evika Silina kwenye mkutano wao mjini Riga, Latvia, Julai 8, 2025. (Picha na Edijs Palens/Xinhua)
Rais Edgars Rinkevics wa Latvia (kulia) na Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani wakihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Riga, Latvia, Julai 8, 2025. (Picha na Edijs Palens/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma