

Lugha Nyingine
Rwanda yasisitiza tena dhamira ya kukuza lugha ya Kiswahili
Rwanda imesisitiza tena dhamira yake ya kukuza lugha ya Kiswahili ikiwa ni sehemu ya juhudi za nchi hiyo kuimarisha mshikamano na udugu wa Afrika.
Akizungumza Jumatatu kwenye ufungaji wa hafla ya maadhimisho ya Miaka Minne ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani mjini Kigali, Waziri wa Elimu wa Rwanda Claudette Irere, amesema Rwanda inatambua umuhimu wa Kiswahili katika kufikia elimu jumuishi na yenye usawa, akibainisha kuwa mwaka 2017 serikali yao iliamua kukiteua Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha rasmi za nchi hiyo, sambamba na Kinyarwanda, Kiingereza na Kifaransa.
Ameongeza kuwa hatua hiyo si tu ni ya kiishara, bali pia ni mkakati madhubuti wa kuiweka Rwanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na eneo pana la lugha za Kiafrika, huku ikiimarisha mshikamano na udugu wa Afrika.
Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki Bi. Caroline Asiimwe amesema kuwa lugha ya Kiswahili ni muhimu katika kujenga jamii, mataifa na kanda ya EAC.
Amesisitiza dhamira ya kamisheni hiyo katika kuwawezesha vijana na uvumbuzi wa kidijitali, akihimiza vijana kumiliki mustakabali wa kidijitali wa Kiswahili na kukitumia kama nyenzo ya ujasiriamali na ujenzi wa amani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma