Ethiopia yaimarisha uhusiano wa kimkakati kupitia mazungumzo ya ngazi ya juu katika Mkutano wa BRICS

(CRI Online) Julai 09, 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Gedion Timothewos amesema mazungumzo ya kimkakati ya kidiplomasia katika Mkutano wa Kilele wa 17 wa BRICS yameimarisha uhusiano wa kimkakati wa Ethiopia na nchi wanachama wa kundi hilo.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatatu, Bw. Timothewos amebainisha kuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alifanya mazungumzo mfululizo ya ngazi ya juu ya kidiplomasia na viongozi wa nchi washirika muhimu pembezoni mwa Mkutano wa Kilele wa 17 wa BRICS, uliofanyika mjini Rio de Janeiro nchini Brazil siku ya Jumapili na Jumatatu.

Timothewos amesema mazungumzo hayo yalitoa fursa muhimu za kuimarisha uhusiano wa pande mbili, huku yakikuza uelewano zaidi na uungwaji mkono katika vipaumbele na mikakati ya maendeleo ya Ethiopia.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje pia amesisitiza azma ya Ethiopia ya kubadilishana uzoefu na nchi wanachama wa BRICS, huku akiorodhesha maeneo ya ushirikiano ambayo Ethiopia inaweza kufaidika na kuchangia, yakiwemo ya uhamishaji teknolojia, ushirikiano wa uwekezaji, na kuchangia maarifa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha