

Lugha Nyingine
Ripoti yaonesha biashara duniani kukua kwa dola bilioni 300 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu huku kukiwa na mtazamo wa kutokuwa na uhakika
Picha hii iliyopigwa tarehe 3 Julai 2025 ikionyesha magari yanayouzwa katika bandari ya Yokohama, Japan. (Xinhua/Jia Haocheng)
GENEVA – Biashara duniani imekua kwa wastani wa dola za kimarekani bilioni 300 katika nusu ya kwanza (H1) ya mwaka 2025, licha ya kasi ukuaji umepungua, Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) limesema katika ripoti yake iliyotolewa jana Jumanne mjini Geneva, Uswizi.
Katika ripoti yake hiyo mpya ya Biashara Duniani, UNCTAD imeonya kwamba mtazamo wa biashara duniani bado una hali ya kutokuwa na uhakika kutokana na kukosekana utulivu wa kisera kunakoendelea, mivutano ya siasa za kijiografia, na dalili za kudhoofika kwa ukuaji duniani katika nusu ya pili ya mwaka.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, biashara duniani iliongezeka kwa takriban asilimia 1.5 katika robo ya kwanza na ilikuwa ikitarajiwa kukua kwa asilimia 2 katika robo ya pili.
Rais Donald Trump wa Marekani akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari kwenye South Lawn ya Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Juni 24, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)
Ripoti hiyo imebainisha kuwa ongezeko la bei lilisababisha kupanda kwa jumla kwa thamani ya biashara, wakati kiasi cha biashara kilikua kwa asilimia 1 tu huku bei za bidhaa zilizouzwa zikiongezeka katika robo ya kwanza na kuendelea kupanda katika robo ya pili.
Inaeleza kuwa, biashara ya huduma ilibaki kuwa kichocheo kikuu cha ukuaji, ikiongezeka kwa asilimia 9 katika robo nne zilizopita.
Ripoti hiyo inaonyesha mwelekeo mchanganyiko katika biashara ya bidhaa miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa katika robo ya kwanza ya 2025, huku uchumi wa nchi zilizoendelea ukizipita nchi zinazoendelea. Ripoti hiyo imehusisha hilo na ongezeko la asilimia 14 la uagizaji bidhaa wa Marekani na ongezeko la asilimia 6 la mauzo ya nje kutoka Umoja wa Ulaya.
“Wakati huo huo, Marekani imeshuhudia kuongezeka kwa nakisi ya biashara katika robo nne zilizopita, ikiongeza kwa kina hali ya kukosekana kwa uwiano wa kibiashara.
Picha hii iliyopigwa kwenye Bandari ya Vancouver ikionyesha kreni ikiinua kontena la mizigo kwenye gati la kontena la Centerm, Vancouver, Canada, Juni 5, 2025. (Picha na Liang Sen/Xinhua)
Ripoti hiyo pia imeonyesha hatari kubwa za mgawanyiko wa kibiashara zilizosababishwa na Marekani kuongeza ushuru hivi karibuni, ikiwemo ushuru wa msingi wa asilimia 10 na ushuru wa ziada unaotozwa kwa chuma na aluminiamu. Imeonya kuwa wimbi jipya la hatua za upande mmoja linaweza kusababisha mivutano ya kibiashara.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma