Rwanda yakaribisha tangazo la amani kati ya DRC na waasi wa M23

(CRI Online) Julai 21, 2025

Rwanda imeeleza kukaribisha kusainiwa kwa tangazo la kanuni kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) mjini Doha, Qatar, likilenga kumaliza mgogoro wa mashariki mwa DRC.

Kufuatia miezi kadhaa ya mazungumzo ya upatanishi yaliyosimamiwa na Qatar, tangazo hilo linaeleza muundo wa kanuni za kimsingi zilizokubaliwa na pande mbili, na kuweka msingi wa mazungumzo endelevu kuelekea makubaliano ya amani ya kina.

Katika taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Rwanda juzi Jumamosi, Rwanda pia imepongeza juhudi za upatanishi za Qatar, ikibainisha kuwa ni mwendelezo wa kazi ya Umoja wa Afrika na mipango mingine ya kikanda.

Imesisitiza kuwa itaendelea kuunga mkono na kuchangia amani na maendeleo katika eneo la Maziwa Makuu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha