China na Misri zatarajia ushirikiano imara zaidi wa Nchi za Kusini kupitia SCO

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 22, 2025

CAIRO - Ubalozi wa China nchini Misri na Kamati ya Mambo ya Nje ya Misri kwa pamoja wamefanya kongamano huko Cairo siku ya Jumapili, wakisisitiza kusukuma mbele kwa hatua madhubuti uhusiano kati ya China na Misri ndani ya mfumo wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO).

Wanadiplomasia waandamizi, wataalam wa mambo ya nje, na wajumbe wa vyombo vya habari kutoka nchi zote mbili wamehudhuria kwenye kongamano hilo.

Katika hotuba yake, Balozi wa China nchini Misri, Liao Liqiang amesema kuwa Misri ni mshirika wa mazungumzo ya SCO, akikaribisha ushiriki kamilifu wa Misri katika shughuli mbalimbali za SCO.

Amesema anatarajia China na Misri zitafanya uratibu na ushirikiano wa karibu chini ya mfumokazi wa SCO, na kuhimiza uhusiano wa pande mbili kuelekea lengo la kujenga jumuiya ya China na Misri yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya na kutoa mchango kwa ajili ya amani na maendeleo ya dunia

Wageni waalikwa kwenye kongamano hilo wamesifu uhusiano unaoendelea katika hali motomoto kati ya Misri na China na jukumu linalofanywa na SCO. Wameelezea matumaini yao kuwa Misri na China zinaweza kutumia fursa za maendeleo zinazotolewa na SCO ili kufanya juhudi za pamoja kuboresha usimamizi wa dunia na kuhimiza ustawi wa Nchi za Kusini.

Ezzat Saad, mkurugenzi wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Misri, ambaye aliongoza kongamano hilo, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba Misri siku zote inajitahidi kuimarisha ushirikiano na China, katika ngazi ya pande mbili na ndani ya mfumo wa SCO.

"Tunaamini kuwa SCO ni jukwaa muhimu la kuhimiza maendeleo ya uhusiano kati ya Misri na China. Misri inatarajia kuimarisha zaidi ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya nchi za Kusini kwenye msingi wa mapendekezo yaliyotolewa na China," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha