Wakulima wa Afrika watumia teknolojia ya Juncao ya China kuboresha uzalishaji uyoga na maisha

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 22, 2025

HUYE, Rwanda - Wataalamu wa kilimo na wakulima wa Afrika wamepongeza mchango wa teknolojia ya Juncao, uvumbuzi wa China kutumika sana katika uzalishaji uyoga na chakula cha mifugo katika nchi mbalimbali za bara hilo.

Innocent Shayamano, mtaalamu mkuu wa kueneza kilimo na mratibu wa mradi kutoka Wizara ya Ardhi, Kilimo, Uvuvi, Maji na Maendeleo ya Vijijini ya Zimbabwe, amesema teknolojia hiyo inabeba jukumu la kimageuzi katika jamii za vijijini za Zimbabwe.

"Teknolojia hii inaweza kuleta mageuzi kwenye maisha. Inaendana na ajenda yetu ya maendeleo ya taifa, hasa Dira ya 2030, ambayo inalenga kuboresha mapato ya familia za vijijini," Shayamano ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua pembezoni mwa warsha kuhusu teknolojia ya Juncao katika Wilaya ya Huye, kusini mwa Rwanda.

Warsha hiyo ilianza Julai 16 na itaendelea hadi Julai 23 katika Kituo cha Kielelezo cha Teknolojia ya Kilimo cha China na Rwanda, ikiandaliwa kwa pamoja na Idara ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya Uchumi na Jamii, Wizara ya Kilimo na Rasilimali za Wanyama ya Rwanda, na Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha Fujian cha China. Inazingatia kujadili matumizi ya teknolojia ya Juncao kwa kilimo cha uyoga, malisho ya mifugo na utunzaji wa mazingira.

Imewakutanisha pamoja maafisa wa kilimo, waelimishaji na wataalam wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

Shayamano, akishiriki kwenye warsha hiyo kwa mara ya pili, pamoja na wakulima watano wa Zimbabwe wanaotafuta kuongeza kwa kina ufahamu wao wa kilimo cha uyoga kinachotegemea Juncao.

Amesema kuwa wakati wakulima wa Zimbabwe kwa kawaida wanatumia mabaki ya pamba kwa kilimo cha uyoga, kupanda kwa gharama ya pamba na kupungua kwa upatikanaji wa pamba kumeifanya isiwe endelevu.

Kinyume chake, nyasi ya Juncao, yenye mavuno ya zaidi ya tani 200 kwa hekta, hutoa mbadala wenye gharama nafuu.

"Huku mabadiliko ya tabianchi yakiathiri upatikanaji wa malisho ya mifugo katika maeneo kavu, nyasi ya Juncao pia inatoa suluhu kwa wakati kwa lishe," Shayamano amesema.

"Ndiyo maana tunafanya kazi kueneza teknolojia hii katika jumuiya nyingi za wakulima," ameongeza.

Zimbabwe na Rwanda ni miongoni mwa nchi kadhaa za Afrika zinazotumia Juncao katika shughuli zao za kilimo.

Abbas Ahmad Umar, mkulima wa Nigeria anayeshiriki kwenye warsha hiyo kwa mara ya kwanza, ameielezea Juncao kama "nyasi ya neema" kutokana na matumizi yake ya mbalimbali.

"Tunaitumia kukuza uyoga, kulisha mifugo, na hata kuzuia mmomonyoko wa udongo. Nitakaporejea Nigeria, ninatumai kuongeza ufahamu kuhusu Juncao, hasa miongoni mwa vijana na wanawake," amesema.

Ikiwa imevumbuliwa nchini China, Juncao -- nyasi chotara -- ni rasilimali ya kilimo yenye kazi nyingi ambayo awali ilitumika katika kilimo cha uyoga. Tangu wakati huo imeonekana kuwa na ufanisi katika kushughulikia tatizo la usalama wa chakula, mapato na changamoto za kimazingira.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha