

Lugha Nyingine
Duru ya 3 ya Mazungumzo kati ya Russia na Ukraine yakubaliana juu ya mabadilishano ya wafungwa, kuwa na maoni tofauti kuhusu usimamishaji vita
Duru ya tatu ya mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine ikifanyika Istanbul, Uturuki, Julai 23, 2025. (Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki/kupitia Xinhua)
ISTANBUL – Wajumbe wa Russia na Ukraine wamefanya duru ya tatu ya mazungumzo ya amani jana Jumatano jioni katika Ikulu ya Ciragan, mjini Istanbul, Uturuki ambapo pande hizo mbili zimeafikiana juu ya kubadilishana mara nyingine tena wafungwa lakini zimepingana juu ya masharti ya kusimamisha vita na uwezekano wa mkutano wa marais.
Msaidizi wa rais wa Russia Vladimir Medinsky na Katibu wa Baraza la Usalama na Ulinzi wa Taifa la Ukraine Rustem Umerov waliongoza wajumbe wa Russia na Ukraine, mtawalia ambapo mazungumzo hayo yaliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan.
Kufuatia mazungumzo hayo yaliyodumu kwa chini ya saa moja, Umerov amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba Ukraine inaendelea kusisitiza juu ya usimamishaji vita kamili na usio wa masharti kama msingi muhimu kwa diplomasia yenye ufanisi.
"Tuko tayari kwa usimamishaji vita sasa na kuanza mazungumzo madhubuti ya amani, na ni juu ya upande mwingine kukubali hatua hii ya msingi kuelekea amani," Umerov amesema, akiongeza kuwa "Tunasisitiza kwamba usimamishaji vita huo lazima uwe halisi. Ni lazima ujumuishe usitishaji kamili wa mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu muhimu".
Kabla ya mazungumzo hayo, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Jumanne kwamba Moscow na Kiev "zina maoni ya tofauti kwa kiasi kikubwa" katika misimamo yao juu ya namna ya kumaliza mgogoro huo, akisema kuwa "kazi kubwa" bado inahitajika kufanywa.
Upande wa Ukraine umependekeza Russia kufanya mkutano kati ya Rais wa Russia Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky "ifikapo mwisho wa Agosti," ambapo ushiriki wa Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan utakuwa "hasa wa thamani," alisema.
Kwenye mkutano mwingine na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Medinsky amesema Russia na Ukraine zimekubaliana kubadilishana wafungwa 1,200 wa vita kila moja, likiwemo pendekezo kutoka Moscow la kubadilishana raia takriban 30 wanaoshikiliwa na Ukraine katika eneo la Kursk.
Russia imerudisha miili ya wanajeshi 7,000 wa Ukraine walifariki na iko tayari kurudisha 3,000 wengine, amesema, ikiomba kurejeshwa kwa idadi yoyote ya wanajeshi wa Russia waliofariki kutoka Ukraine.
Kuhusu mkutano wa kati ya marais Putin na Zelensky uliopendekezwa na Ukraine, Medinsky amesema mkutano kama huo hauko unatiliwa maanani hadi michakato fulani ikamilike.
Wakati huo huo, Zelensky ameandika kwenye jukwaa la kijamii la X baada ya mazungumzo hayo kwamba hatua ya tisa ya kubadilishana wafungwa imefanyika "leo," (jana Jumatano) ambayo ilihusisha watu zaidi ya 1,000 kutoka upande wa Ukraine, wakiwemo wale "wanaoumwa sana na waliojeruhiwa vibaya."
"Ni muhimu kwamba mabadilishano bado yanaendelea," ameandika.
Duru ya tatu ya mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine ikifanyika Istanbul, Uturuki, Julai 23, 2025. (Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki/kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma