

Lugha Nyingine
Thailand na Cambodia zakubaliana juu ya usimamishaji vita "bila masharti"
Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim (katikati), Waziri Mkuu wa Cambodia, Hun Manet (kushoto) na Kaimu Waziri Mkuu wa Thailand, Phumtham Wechayachai wakipeana mikono mjini Putrajaya, Malaysia, Julai 28, 2025. (Bernama kupitia Xinhua)
PUTRAJAYA, Malaysia - Viongozi wa Thailand na Cambodia wamekubaliana kutekeleza usimamishaji vita kuanzia usiku wa manane jana Jumatatu, Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim amesema kufuatia mkutano maalum wa kusimamisha vita uliofanyika kati ya Waziri Mkuu wa Cambodia Hun Manet na Kaimu Waziri Mkuu wa Thailand Phumtham Wechayachai ukiongozwa na Anwar mapema Jumatatu mchana kwenye makazi ya Waziri Mkuu wa Malaysia mjini Putrajaya, Malysia.
Balozi wa China nchini Malaysia Ouyang Yujing alihudhuria na kuhutubia mkutano huo.
Kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari kufuatia mazungumzo juu ya kusimamisha vita, Anwar ameelezea mchakato wa hatua kwa hatua wa kutuliza hali na utaratibu ambao kupitia kwao utatekelezwa na kufuatiliwa.
"Zote Cambodia na Thailand zimefikia maelewano ya pamoja kama ifuatavyo – usimamishaji vita usio na masharti utatekelezwa mara moja kuanzia saa 6:00 (saa za nchi husika) tarehe 28 Julai 2025. Hii ni hatua muhimu ya kwanza kutuliza hali na kurejesha amani na usalama," amesema.
Kwa mujibu wa Anwar, usimamishaji vita wa awali utafuatiwa na kuanzishwa tena kwa mawasiliano kati ya makamanda wa jeshi wa maeneo husika kwa pande zote mbili kupitia mkutano wa ana kwa ana saa 1 asubuhi (kwa saa za huko) leo Julai 29, ambao utafuatiwa na mkutano wa maofisa wa ulinzi wa pande zote mbili, ukiongozwa na mwenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini-Mashariki (ASEAN), kama pande zote mbili zinakubaliana, na hatimaye mkutano Kamati ya Mpaka wa Jumla (GBC) Agosti 4 ambao utaandaliwa na Cambodia.
"Ikiwa mwenyekiti wa zamu wa ASEAN, Malaysia iko tayari kuratibu timu ya waangalizi ili kujiridhisha na kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano hayo ya usimamishaji vita. Malaysia pia itashauriana na nchi wanachama wa ASEAN kushiriki katika juhudi za uangalizi, ikionyesha dhamira ya kikanda kuunga mkono amani katika maeneo ya kanda," amesema.
"Pande zote mbili pia zimekubaliana kurejesha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mawaziri wakuu, mawaziri wa mambo ya nje na mawaziri wa ulinzi," Anwar ameongeza.
Hun Manet amesema mazungumzo hayo yenye mafanikio yatatoa fursa nyingi kwa mamia kwa maelfu ya watu wa pande zote mbili kurejea katika hali ya kawaida na kumaanisha mwanzo wa juhudi za kujenga upya hali ya kuaminiana, imani na ushirikiano kati ya Cambodia na Thailand.
Kwa upande wake, Phumtham amesema kuwa matokeo yaliyopatikana katika mkutano huo yanaonyesha nia ya Thailand kwa utatuzi wa amani wakati huohuo ikiendelea kulinda mamlaka ya nchi hiyo na maisha ya watu wa Thailand.
"Tumekubaliana kusimamisha vita ambako kutatekelezwa kwa mafanikio katika nia njema na pande zote mbili," ameongeza.
Tangu mapigano kati ya wanajeshi wa Cambodia na Thailand juu ya maeneo ya mpaka yenye mzozo yalipozuka Alhamisi wiki iliyopita, watu zaidi ya 30 wameshauawa kutoka pande zote mbili, na watu zaidi ya 100,000 wamehamishwa hadi maeneo salama, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na nchi hizo mbili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma