Viongozi wa kimataifa wahimiza hatua za dharura juu ya changamoto za mfumo wa chakula

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 29, 2025

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres akihutubia Mkutano wa Kilele wa Pili wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula kwa njia ya video mjini Addis Ababa, Ethiopia, Julai 28, 2025. (Xinhua/Michael Tewelde)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres akihutubia Mkutano wa Kilele wa Pili wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula kwa njia ya video mjini Addis Ababa, Ethiopia, Julai 28, 2025. (Xinhua/Michael Tewelde)

ADDIS ABABA - Viongozi wa kimataifa jana Jumatatu kwenye Mkutano wa pili wa Kilele wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula, unaoendelea katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, wametoa wito wa hatua za pamoja kushughulikia changamoto zinazokabili mifumo ya chakula.

Mkutano huo, unahudhuriwa na viongozi wa kisiasa kutoka kote duniani, wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kikanda, vilevile wawakilishi kutoka sekta binafsi na mashirika ya kiraia, ili kudhamiria tena kwa majukumu yao ya pamoja.

Akihutubia kikao cha ufunguzi rasmi siku hiyo ya Jumatatu, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) Mahmoud Ali Youssouf amesisitiza haja ya kuifanyia mageuzi mifumo ya chakula duniani ili kukabiliana na changamoto muhimu za maendeleo endelevu.

"Mageuzi ya mifumo ya chakula si tu hitaji la kimaadili. Ni hitaji muhimu la kimkakati katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa kumaliza njaa, kupunguza umaskini, na kujenga uchumi unaohimili tabianchi," amesema.

Mkuu huyo wa AUC amezungumzia "hatua ngumu" za Afrika katika mageuzi ya mifumo ya chakula, zikiungwa mkono na dhamira za pamoja za bara na malengo ya uwekezaji ili kujenga mifumo ya chakula iliyo himilivu, jumuishi na iliyo ya kisasa kuhimili tabianchi.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza haja muhimu ya kutimiza ahadi za pamoja katika kuhakikisha mifumo ya chakula duniani ambayo ni jumuishi, endelevu, yenye usawa, himilivu na inayojikita katika haki za binadamu.

"Njaa duniani inaongezeka, mishtuko ya kibiashara inasukuma bei za chakula nje ya uwezo wa kumudu, na theluthi moja ya watu duniani hawawezi kumudu mlo wenye afya huku theluthi moja ya chakula duniani kikipotea au kutupwa," Guterres amesema, akionya kuwa mabadiliko ya tabianchi na migogoro vinaongeza zaidi njaa duniani kote.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni amesisitiza haja ya kushughulikia vichocheo vikubwa vya ukosefu wa usalama wa chakula duniani. Amesema kuwa ingawa ukosefu wa usalama wa chakula umepungua kwa kiasi kikubwa katika miongo kadhaa iliyopita, jambo hilo bado linaathiri takriban asilimia 10 ya watu duniani.

Akiuelezea ukosefu wa usalama wa chakula kama suala muhimu la kisiasa na kiuchumi duniani, ameonya juu ya matokeo ya kijanga, yakiwemo ya umaskini na migogoro, kwani jamii zinakuwa dhaifu zaidi kwa vurugu, ugaidi, na uhamiaji wa kulazimishwa.

Akiunga mkono maoni hayo, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha ufadhili unaotabirika ili kuunga mkono uwekezaji katika kilimo, mageuzi vijijini, miundombinu, na lishe barani Afrika na kwingineko.

Mkutano huo, unaofanyika kuanzia Julai 27 na umepangwa kumaliza leo Julai 29, unajikita katika kutafakari upigaji hatua wa kimataifa kwenye mageuzi ya mifumo ya chakula, kuimarisha ushirikiano, na kufungua ufadhili na uwekezaji ili kuharakisha hatua kuelekea SDGs za Umoja wa Mataifa.

Washiriki wakihudhuria Mkutano wa Kilele wa Pili wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula mjini Addis Ababa, Ethiopia, Julai 28, 2025. (Xinhua/Michael Tewelde)

Washiriki wakihudhuria Mkutano wa Kilele wa Pili wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula mjini Addis Ababa, Ethiopia, Julai 28, 2025. (Xinhua/Michael Tewelde)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha