Jeshi la Nigeria laua viongozi wa ngazi ya juu wa ISWAP katika shambulizi la anga

(CRI Online) Julai 29, 2025

Makamanda kadhaa waandamizi na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu la Jimbo la Afrika Magharibi (ISWAP) wameuawa katika mashambulizi mfululizo ya anga yaliyofanywa na Jeshi la Nigeria katika eneo la Ziwa Chad.

Katika taarifa yake iliyotolewa Jumatatu, msemaji wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Nigeria, Ehimen Ejodame, amesema kikosi cha kupambana na ugaidi, kinacholenga kuangamiza uongozi wa kundi hilo la kigaidi, kilishambulia Arina Woje, eneo linalotambulika kama ngome ya ISWAP katika eneo la Tumbuns Kusini mwa Borno, karibu na Ziwa Chad.

Ameeleza kuwa shambulizi hilo la anga limekuja kufuatia mfululizo wa taarifa za kijasusi, uchunguzi na upelelezi ambao ulithibitisha kurejea kwa magaidi katika eneo hilo baada ya mapigano ya hivi karibuni baina ya makundi.

ISWAP imekuwa ikishirikiana na kundi la Boko Haram katika jaribio la kuanzisha Jimbo la Kiislamu kaskazini mashariki mwa Nigeria. Makundi hayo ya kigaidi pia yamekuwa yakiendeleza mashambulizi yao hadi katika nchi nyingine kwenye Bonde la Ziwa Chad.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha