Rais wa Kenya asaini sheria mpya ya kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi

(CRI Online) Julai 31, 2025

Rais wa Kenya William Ruto amesaini Mswada wa Mgongano wa Maslahi kuwa sheria jana Alhamisi ili kusaidia kuimarisha vita dhidi ya ufisadi nchini.

Kwenye taarifa iliyotolewa mjini Nairobi baada ya kusainiwa mswada huo, Ruto amesema sheria hiyo mpya inayobatilisha Sheria ya Maadili ya Maafisa wa Umma, inaleta muundo wa kina wa kudhibiti migongano ya kimaslahi serikalini ili kudhibiti matumizi mabaya ya mamlaka ya maafisa wa umma, kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Aidha Ruto amesisitiza kuwa sheria hiyo mpya inaweka sheria wazi ili kuhakikisha maafisa wa umma wanahudumu kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji.

Amebainisha kuwa sheria hiyo mpya pia inawapa Wakenya fursa ya kuwawajibisha maafisa wa umma katika kutekeleza mamlaka yao.

Sheria hiyo inaipa mamlaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ya kusimamia utekelezwaji wake, na chombo hicho cha kupambana na ufisadi kitashughulikia masuala yanayohusiana na kutangaza mali kwa maafisa wote wa umma, si tu kwa Watendaji Wakuu bali pia hata katika Bunge na Mahakama.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha