Kenya na Uganda zasaini makubaliano manane mapya ya kibiashara

(CRI Online) Julai 31, 2025

Kenya na Uganda zimetiliana saini hati nyingine nane za maelewano (MoUs) jana Jumatano mjini Nairobi, Kenya, chini ya mikataba 17 ambayo tayari ipo, ili kuimarisha ushirikiano wa kisheria na kitaasisi katika sekta za kimkakati.

Hafla ya utiaji saini huo ilishuhudiwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliyezuru nchini humo na mwenzake wa Kenya William Ruto.

Akizungumza na wanahabari Ruto alisema makubaliano hayo ya ushirikiano kati ya Shirika la Taifa la Takwimu la Kenya na Bodi ya Taifa ya Takwimu ya Uganda yametiwa saini ili kuimarisha mabadilishano ya maarifa ya kisayansi na kiufundi.

Kwa upande wake, Museveni alisisitiza kuwa uchumi wa kisasa unachochewa na uzalishaji wa bidhaa na huduma, akihimiza vijana kujikita katika kutumia fursa kubwa ya soko la Afrika.

Ruto na Museveni wameahidi kufanya juhudi za kuimarisha taasisi za kikanda na kuendeleza malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiwemo kupiga hatua kuelekea umoja wa forodha, soko la pamoja, sarafu moja na shirikisho la kisiasa.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha