Uganda yaipongeza China kwa kuunga mkono amani na utulivu katika Pembe ya Afrika

(CRI Online) Julai 31, 2025

Uganda imeipongeza China kwa kuunga mkono juhudi za kikanda za kuhimiza amani na utulivu katika Pembe ya Afrika.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda John Mulimba siku ya Jumanne kwenye Mkutano wa tatu wa Amani na Maendeleo ya Pembe ya Afrika, uliofanyika mjini Kampala, Uganda.

Mulimba alisema katika hotuba yake kuwa China imekuwa ikiunga mkono mapendekezo yanayoangazia mazungumzo ya kikanda na kutatua matatizo, akibainisha kuwa eneo hilo linaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo ukosefu wa usalama, matishio ya kuvuka mipaka, mashinikizo ya kimazingira na hali tete ya kiuchumi.

Ameongeza kuwa katika mazingira hayo, Pendekezo la Usalama wa Dunia (GSI) lililotolewa na China limechangia ipasavyo katika mazungumzo ya kimataifa kuhusu usalama wa pamoja, likiangazia mazungumzo, kuheshimu mamlaka ya taifa, na mbinu za kina za kushughulikia migogoro kwa kuendana na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063, hasa matarajio ya Afrika kuwa bara lenye amani na usalama.

Waziri huyo pia amelisifu Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia (GCI) lililotolewa na China, akilielezea kuwa "mfumo wa maono unaotaka watu kukumbatia maadili ya kuheshimiana, mabadilishano ya kiutamaduni na uwajibikaji wa pamoja".

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha