Rais wa Tanzania aweka jiwe la msingi la ujenzi wa eneo maalum la viwanda la Kwala

(CRI Online) Agosti 01, 2025

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Eneo Maalum la Kiviwanda la Kwala, lililopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Eneo hilo maalum ni mradi wa ubia wa kampuni sita, likiwa linajengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 2,500 na likitarajiwa kuwa na viwanda zaidi ya 200.

Mkuu wa eneo hilo maalum Bw. Janson Huang amesema mradi huo unalenga kuifanyia mageuzi Tanzania kuwa kitovu kinachoongoza kwa biashara, uzalishaji wa kiviwanda na uvumbuzi wa nishati safi.

Bw. Huang amesema tayari kuna viwanda 12, saba kati ya hivyo vinafanya kazi na vitano vinaendelea kujengwa, na kwamba kwa sasa eneo hilo maalum limeajiri zaidi ya watanzania 1,000, idadi ambayo inatarajiwa kufikia 5,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka kesho.

Miongoni mwa malengo ya siku za baadaye ni eneo hilo maalum ni kuunga mkono utengenezaji wa betri za magari ya umeme, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kupunguza uzalishaji wa kaboni ifikapo 2050.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha