Maonyesho ya Picha ya kuadhimisha Miaka 80 tangu China kupata ushindi katika Vita dhidi ya Uvamizi wa Japan yafanyika nchini Russia (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 04, 2025
Maonyesho ya Picha ya kuadhimisha Miaka 80 tangu China kupata ushindi katika Vita dhidi ya Uvamizi wa Japan yafanyika nchini Russia
Mfanyakazi akielezea picha kwa watembeleaji katika maonyesho ya picha ya kumbukumbu ya miaka 80 tangu kupata ushindi katika Vita vya Watu wa China dhidi ya Uvamizi wa Japan na Vita vya Dunia vya Kupinga Ufashisti mjini Vladivostok, Russia, Septemba 2, 2025. (Picha na Guo Feizhou/Xinhua)

VLADIVOSTOK - Maonyesho ya picha yenye kaulimbiu ya "Marafiki wa Kweli Walioanzia Motoni" yamefunguliwa juzi Jumanne mjini Vladivostok, Russia ili kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 tangu kupata ushindi katika Vita vya Watu wa China dhidi ya Uvamizi wa Japan na Vita vya Dunia vya Kupinga Ufashisti.

Maonyesho hayo yameandaliwa kwa pamoja na Konsuli Kuu ya China mjini Vladivostok, Ofisi ya Kanda ya Eurasia ya Shirika la Habari la China, Xinhua, Shirika la Picha la China na Tawi la Mashariki ya Mbali la Akademia ya Sayansi ya Russia.

Watu zaidi ya 300 walihudhuria hafla ya ufunguzi wa maonyesho hayo, wakiwemo wakilishi kutoka sekta za kisiasa, biashara na kitaaluma katika Eneo la Primorye, vilevile wajumbe kutoka nchi mbalimbali na wanajumuiya ya Wachina nchini Russia.

Maonyesho hayo yanajumuisha picha zaidi ya 60 za thamani kutoka kwenye makavazi ya Xinhua, zikiangazia mapambano ya pamoja ya wanajeshi na raia wa China na Soviet dhidi ya uvamizi wa kifashisti, vilevile urafiki mkubwa ulioundwa wakati wa vita.

Wang Jun, kaimu konsuli mkuu wa China mjini Vladivostok, amesema katika hafla ya ufunguzi kwamba China ilikuwa uwanja mkuu wa vita katika Mashariki wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, akibainisha kuwa watu wa China na Soviet walipigana bega kwa bega na kuunda uhusiano wa karibu wa ukamarade katika mapambano yao ya maisha na kifo.

"Kila picha ya thamani inaturudisha nyuma katika miaka hiyo ya vita, ikituruhusu kuwaenzi mashujaa wa kike na kiume waliojitoa mhanga maisha yao kwa ajili ya uhuru na haki, na kukumbuka historia iliyoandikwa kwa damu na ujasiri." amesema Wang.

Vera Shcherbina, makamu gavana wa kwanza na mwenyekiti wa serikali ya Eneo la Primorye, amesisitiza kuwa Russia na China zina msimamo mmoja juu ya kutetea kumbukumbu za kihistoria na kulinda utaratibu wa kimataifa wa baada ya vita.

"Maonyesho haya yatasaidia kuongeza maelewano na urafiki unaoendelea kati ya watu wa Russia na China." amesema.

Katika barua yake ya pongezi, Gennady Krasnikov, mkuu wa Akademia ya Sayansi ya Russia, amesisitiza umuhimu wa kipekee wa maonyesho hayo wakati ambapo China na Russia zikiadhimisha kwa pamoja miaka 80 tangu kupata ushindi huo.

"Yanatumika kama hatua muhimu kwa nchi zote mbili kukumbuka na kurithisha historia…Historia yetu ya pamoja itarekodiwa milele, na utukufu wa ushindi utahamasisha mafanikio mapya." ameandika.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha