Rais wa Rwanda ahimiza anga wazi wakati mkutano wa kilele wa usafiri wa anga barani Afrika ukianza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 05, 2025
Rais wa Rwanda ahimiza anga wazi wakati mkutano wa kilele wa usafiri wa anga barani Afrika ukianza
Wateja wawili wakishauriana na waonyeshaji kwenye Mkutano wa Kilele na Maonyesho ya 9 ya Usafiri wa Anga barani Afrika mjini Kigali, Rwanda, Septemba.4, 2025. (Picha na Cyril Ndegeya/Xinhua)

KIGALI - Mkutano wa Kilele na Maonyesho ya 9 ya Usafiri wa Anga barani Afrika umefunguliwa jana Alhamisi mjini Kigali, mji mkuu wa Rwanda, ukitoa wito kwa nchi za Afrika kufungua anga na kuwekeza katika sekta ya anga yenye nguvu na ustawi zaidi ambapo mkutano huo umevutia wawakilishi kutoka mashirika ya ndege, viwanja vya ndege, mamlaka za anga, na wataalamu wa tasnia kutoka bara zima na kwingineko.

Akifungua mkutano huo, Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema kuwa gharama kubwa za usafiri wa anga bado ni kikwazo kwa utalii na mawasiliano barani Afrika.

Akisema kuwa anga za Afrika lazima zifunguliwe ili kuwahudumia vyema wananchi, wafanyabiashara, na uchumi mpana, Rais Kagame amehimiza serikali na viongozi wa sekta hiyo kushirikiana ili kufanya usafiri wa anga kuwa nafuu na endelevu zaidi.

"Utalii wa ndani ya Afrika ni asilimia 15 tu. Kwa nini? Kwa sababu usafiri wa anga ni ghali," amesema.

“Licha ya kukua kwa kasi kwa mahitaji, Afrika inachukua chini ya asilimia 5 ya usafiri wa anga duniani,” Kagame amesema, akiongeza kuwa kwa anga ya Afrika kuwa jumuishi kweli, na ili viwanja vyetu vya ndege na sekta ya usafiri wa anga kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi, ni lazima tujipange, tuwekeze katika miundombinu, na kukumbatia teknolojia.

"Ifikapo 2044, wakati usafiri wa anga unatarajiwa kuongezeka maradufu, tunapaswa kuwa tayari na anga ambazo ni salama na fanisi, na upekee wa nafasi ya anga ya Afrika ambayo ni jumuishi," amesema.

Kagame pia alitembelea maonyesho hayo, ambayo yanashirikisha waonyeshaji hadi 100 wanaoonyesha mchango wao katika ukuaji wa usafiri wa anga barani humo.

Mkutano huo wa kilele wa siku mbili, unaohitimishwa leo Ijumaa, unafanyika chini ya kaulimbiu ya "Kushirikiana kufungua ukuaji wa Afrika – Ni kwa namna gani Afrika inaweza kutoa sekta endelevu ya usafiri wa anga?" 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha