Lugha Nyingine
Kituo cha Huduma za Kimataifa cha Nanshan, Shenzhen chasaidia Kampuni za China Kwenda Kimataifa
![]()  | 
| Waandishi wa habari wakitazama bango ukutani linaloeleza huduma mbalimbali zinazotolewa na Kituo cha Huduma za Kimataifa “Go Global” cha Nanshan, Shenzhen, China. (Picha/People’s Daily Online) | 
Kituo cha Huduma za Kimataifa cha Nanshan "Go Global" ("Kusaidia Kampuni za China Kwenda Kimataifa") chenye makao yake makuu katika Eneo la Nanshan, mjini Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, kusini mwa China kimekuwa ni daraja muhimu linalowezesha kampuni za Shenzhen na sehemu nyingine za China kwenda kufanya biashara katika nchi na maeneo mbalimbali duniani kupitia "sera ya kwenda kimataifa".
Aidha, kituo hicho ambacho kilianzishwa na kufunguliwa rasmi mwaka huu Aprili 29 na Serikali ya Eneo la Nanshan pia kinajikita katika kusaidia na kuunga mkono kampuni za kigeni ambazo zinatafuta kuingia kwenye soko la China.
Kikiwa kinaongozwa na filosofia ya "uongozi wa serikali, ushirikiano na kampuni, huduma zinazotegemea jukwaa" kituo hicho hutoa huduma zote katika sehemu moja na uungaji mkono wa mambo yote, kikilenga kufanya kazi kama makao makuu ya kimataifa kwa kampuni hizo za China na za kigeni zinazotumia jukwaa lake.
Xu Sijie, Mkurugenzi na Meneja Mkuu wa kituo hicho, akizungumza na waandishi wa habari wa Timu ya Kufanya Utafiti Kuhusu Shenzhen ya People's Daily Online jana Alhamisi kwenye makao yake makuu amesema kuwa, kituo chake hutoa huduma zinazojikita katika mambo kama vile kampuni za China kwenda kimataifa, huduma za taarifa na kukutanisha kampuni zenye kuhitajiana.
Amezitaja huduma kumi za msingi zinazotolewa na kituo hicho kuwa ni: huduma za kimataifa za kisheria, huduma za mambo ya fedha za kuvuka mpaka, huduma za uvumbuzi wa teknolojia, huduma za ushauri wa kimkakati, huduma za intelijensia ya kibiashara, ushauri wa kodi na mapato duniani, huduma za maeneo maalum ya ng'ambo, huduma za vipaji duniani, huduma za kufanya chapa kuwa za kimataifa, na huduma za biashara ya kuvuka mpaka.
Amesema kuwa, kampuni ambazo wanalenga kuzisaidia zitakuwa zikipata manufaa mbalimbali yakiwemo, kuunganishwa na rasilimali duniani, kuwa katika mduara mzima wa uungwaji mkono kwenda kimataifa, kuwekwa kwenye mfumo wa ulinzi wa hakimiliki, kufanya maamuzi yenye kuongozwa na data, mwitikio wa haraka wa mahitaji, na kuingia katika mtandao wa kimataifa wa uvumbuzi.
"Kwa sasa kituo kimeshaweka sehemu moja rasilimali za huduma za kitaalam zaidi ya 210 zinazohusu usajili na utoaji vyeti, utafiti wa soko, rasilimali watu, huduma za mambo ya fedha na kodi, mashauri ya kisheria, utangazaji wa chapa, uchukuzi katika minyororo ya usambazaji bidhaa, na huduma nyingine muhimu 12 za kuunganisha" amesema.
Kuhusu kampuni za kigeni zinazoingia soko la China, Xu amesema, wanazisaidia katika mwongozo wa matumizi ya sera, ufuataji sheria na ubainishaji hatari, uhusiano wa umma na wenyeji, mawasiliano kuhusu mashauri ya kisheria, usimamizi wa mtaji wa kuvuka mpaka na mambo mengine mengi.
Ukiwa ni mji mwanzilishi na mfano kwa sera za kufungua mlango na "kwenda kimataifa" za China, Shenzhen umeanzisha taasisi na mashirika mbalimbali kuhakikisha na kudumisha mafanikio ya sera hizo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




