Waziri Mkuu wa China atoa wito kwa Bunge la Marekani kuwezesha mazungumzo na ushirikiano wa pande mbili

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 22, 2025

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na ujumbe wa Bunge la Marekani kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Septemba 21, 2025. (Xinhua/Liu Weibi)

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na ujumbe wa Bunge la Marekani kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Septemba 21, 2025. (Xinhua/Liu Weibi)

BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amekutana na ujumbe wa Bunge la Marekani mjini Beijing jana Jumapili, akitoa wito kwa Bunge la Marekani kuitazama China na uhusiano wa pande mbili kwa njia sahihi, kujitahidi kuwezesha mazungumzo na ushirikiano, na kufanya kazi ya kiujenzi katika kuimarisha urafiki kati ya China na Marekani na maendeleo ya pamoja.

Alipokutana na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Li amesema kuwa China na Marekani ni nchi kubwa zenye ushawishi mkubwa duniani na kwamba kudumisha maendeleo tulivu, mazuri na endelevu ya uhusiano wa pande mbili kunaendana na maslahi ya pamoja ya pande zote mbili na kukidhi matarajio ya jumuiya ya kimataifa.

“Rais Xi Jinping wa China na Rais Donald Trump wa Marekani wamefanya mazungumzo kadhaa kwa njia ya simu mwaka huu na kufikia maafikiano kwamba China na Marekani zinapaswa kuimarisha mazungumzo na ushirikiano, wakitoa mwongozo wa kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya uhusiano wa pande mbili katika hatua inayofuata,” Li amesema.

Amesema China inapenda kushirikiana na Marekani ili kufikia kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na kufanya ushirikiano wa kunufaishana, na inatumai Marekani itashirikiana na China katika mwelekeo huo huo ili kusukuma mbele uhusiano wa pande mbili kwenye njia sahihi, na kuzinufaisha nchi hizo mbili na dunia kwa ujumla.

Waziri Mkuu huyo amesema kuwa China na Marekani zinapaswa kuwa washirika wa kujiendeleza kwa pamoja, kutendeana kwa udhati, kuwezeshana, na kufikia kufanikishana.

Ameongeza kuwa, China inapenda kushirikiana na Marekani kushughulikia matatizo ya kila mmoja wao kwa njia ya mawasiliano katika moyo wa usawa, kuheshimiana na kunufaishana.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha