Sudan yalaani kundi la RSF kwa shambulizi la mabomu dhidi ya msikiti mjini El Fasher na kusababisha vifo zaidi ya 70

(CRI Online) Septemba 22, 2025

Serikali ya Sudan imelaani wanamgambo wa Vikosi vya Mwitikio wa Haraka (RSF) kwa kufanya shambulizi la mabomu dhidi ya msikiti mjini El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini wakati wa sala ya alfajiri na kusababisha vifo visivyopungua 70.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imelielezea shambulizi hilo kuwa ni "uvamizi katili wa kigaidi" na ni ukiukaji mkubwa wa kanuni za kidini na mikataba ya kimataifa inayolinda raia na maeneo ya ibada, ikitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya "ugaidi unaolenga raia wasio na silaha."

Kwa mujibu wa habari kutoka makundi ya kujitolea mjini El Fasher, droni iliyodhibitiwa na kundi la RSF ilitumika katika shambulizi hilo dhidi ya msikiti.

Hadi wakati habari hii inachapishwa, kundi la RSF lilikuwa bado halijatoa kauli yoyote kuhusu shambulizi hilo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha