Lugha Nyingine
OECD yapandisha makadirio yake ya ukuaji uchumi duniani kwa nusu ya kwanza ya mwaka huu
Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) jana Jumanne lilitoa ripoti ya katikati ya mwaka ya hali na mtazamo wa uchumi duniani, ikikadiria kuwa uchumi duniani utakua kwa asilimia 3.2 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.3 kuliko makadirio yaliyotolewa mwezi Juni.
Shirika hilo limesema katika ripoti yake hiyo kwamba, kasi ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2026 inakadiriwa kushuka hadi asilimia 2.9, ikiwa ni sawa na makadirio ya mwezi Juni.
Ripoti hiyo inasema, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, ukuaji wa uchumi duniani umeonesha uhimilivu mkubwa zaidi kuliko ilivyotarajiwa, hasa katika masoko yanayoibukia.
Imeeleza kuwa, athari za sera ya ushuru ya Marekani hazijaonekana kikamilifu, na zinasambaa hadi kwenye maamuzi ya matumizi, soko la nguvukazi na bei ya bidhaa za matumizi.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa, uchumi duniani bado unakabiliwa na hatari kubwa, ambapo vipengele kadhaa ikiwemo kuongezeka kwa ushuru, mfumko wa bei, wasiwasi kuhusu hatari za mambo ya fedha na tathmini mpya kuhusu hatari za soko la mambo ya fedha, vyote vinaweza kupunguza makadirio hayo ya ongezeko la uchumi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



