Lugha Nyingine
Wakenya 255 wafariki kwenye mgogoro unaoongezeka kati ya binadamu na wanyamapori ndani ya miaka miwili
Kenya imerekodi matukio 26,641 yaliyotokea kati ya wanyamapori na binadamu katika miaka miwili iliyopita, ambayo yamesababisha vifo vya watu 255 huku yakiendelea kuongezeka.
Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS), Erustus Kanga, amesema katika taarifa yake iliyotolewa Jumanne wiki hii jijini Nairobi kwamba matukio hayo yalirekodiwa kati ya Julai 2023 na Juni 2025.
Kanga pia amesema kulikuwa na watu 725 waliojeruhiwa, mashamba 9,300 yaliyovamiwa, kesi 5,200 za wanyamapori kuwinda mifugo, zaidi ya matukio 1,000 ya uharibifu wa mali, na matishio karibu 10,000 ya moja kwa moja.
Ameongeza kuwa namba hizo zinaonyesha mgogoro unaoathiri maisha, riziki, na mustakabali wa uhifadhi wa mazingira nchini Kenya.
Afisa huyo wa KWS amebainisha kuwa, ili kupunguza mgogoro huo, shirika hilo la wanyamapori linatekeleza mikakati kadhaa, ikiwemo kuhifadhi na kurejesha maeneo yaliyoharibiwa, kulinda njia za uhamaji wanyama, kuimarisha fidia, kuboresha vyanzo vya riziki kupitia uchumi wa wanyamapori na biashara za kitamaduni, na kuweka mifumo ya kutoa tahadhari mapema, droni, na kufuatilia maeneo yenye hatari kwa wakati.
Kwa mujibu wa KWS, sababu za kuongezeka kwa mgogoro huo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, ambayo yameathiri upatikanaji wa maji, na pia ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko katika matumizi ya ardhi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



