Sanae Takaichi achaguliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Japan (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 22, 2025
Sanae Takaichi achaguliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Japan
Sanae Takaichi (wa pili kulia, mbele) akionekana kwenye kikao maalum cha Baraza la Wawakilishi mjini Tokyo, Japan, Oktoba 21, 2025. (Xinhua/Jia Haocheng)

TOKYO - Sanae Takaichi, kiongozi wa chama tawala nchini Japan cha Liberal Democratic (LDP), amechaguliwa rasmi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo jana Jumanne baada ya kushinda katika mabaraza yote mawili, na kuwa kiongozi wa kwanza mwanamke nchini humo.

Kwenye upigaji kura wa Baraza la Wawakilishi, Takaichi amepata kura 237, na kumshinda kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha Constitutional Democratic Yoshihiko Noda aliyepata kura 149 na wagombea wengine washindani.

Baraza la Madiwani pia lilifanya shughuli yake ya kupiga kura, lakini hakuna mgombea aliyepata kura nyingi kuamua mshindi katika duru ya kwanza. Takaichi aliongoza kwa kura 123, akifuatiwa na Noda aliyepata kura 44.

Kutokana na hali hiyo, upigaji kura wa marudio ambao haujawahi kushuhudiwa katika baraza la juu, wa kwanza katika miaka 13, ulianzishwa kati ya Takaichi na Noda, na Takaichi hatimaye kushinda kinyang’anyiro.

Kwa kushinda katika mabaraza yote mawili, ametangazwa rasmi kuwa waziri mkuu wa 104 wa Japan, mwanamke wa kwanza katika taifa hilo kushika wadhifa huo.

Takaichi alikuwa akitarajiwa kukamilisha safu yake ya baraza la mawaziri, kushiriki katika hafla ya uthibitisho, na kuzindua baraza jipya la mawaziri baadaye siku hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha