Lugha Nyingine
Waziri wa Mambo ya Nje wa China atumai China na Marekani zitajenga mazingira kwa maendeleo ya uhusiano wa pande mbili
BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi ameelezea matumaini yake kwamba China na Marekani zitafanya kazi katika mwelekeo mmoja ili kujiweka tayari vizuri kwa mazungumzo ya ngazi ya juu na kujenga mazingira kwa maendeleo ya uhusiano wa pande mbili.
Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ameyasema hayo katika mazungumzo kwa njia ya simu jana Jumatatu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio.
Amesema uhusiano kati ya China na Marekani una athari kwa dunia nzima, na uhusiano mzuri, tulivu na endelevu wa pande mbili unahudumia maslahi ya muda mrefu ya nchi zote mbili na unakidhi matarajio ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa.
"Rais Xi Jinping na Rais Donald Trump wote ni viongozi muhimu duniani ambao wamedumisha mawasiliano ya muda mrefu na kuheshimiana, hali ambayo imekuwa jambo muhimu zaidi la kimkakati katika uhusiano kati ya China na Marekani," Wang amesema.
"Awali, uhusiano wa kiuchumi na biashara kati ya China na Marekani umekumbana na misuguano mipya," Wang amesema, akiongeza kuwa kupitia mazungumzo yaliyofanyika Kuala Lumpur, pande hizo mbili zimefafanua misimamo yao, zimeongeza kuelewana, na kufikia maafikiamo ya mfumokazi juu ya kushughulikia masuala ya dharura ya kiuchumi na biashara kwa msimamo wenye usawa.
"Hii kwa mara nyingine tena inathibitisha kwamba inawezekana kutuliza na kusukuma mbele uhusiano wa pande mbili ilimradi tu pande hizo mbili zitekeleze kikamilifu maafikiano muhimu yaliyofikiwa na wakuu hao wawili wa nchi, kushikilia kanuni za usawa, kuheshimiana na kunufaishana, kutatua tofauti kupitia mazungumzo, na kujizuia kutumia shinikizo," Wang amesema.
Kwa upande wake, Rubio amesema uhusiano kati ya Marekani na China ni uhusiano muhimu zaidi wa pande mbili duniani, na anatazamia kutuma ishara chanya kwa dunia kupitia mazungumzo ya ngazi ya juu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



