Uturuki yasaini makubaliano kununua ndege 20 za kivita za Eurofighter Typhoon kutoka Uingereza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 28, 2025

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kulia) na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer wakionyesha nyaraka za makubaliano zilizosainiwa  huko Ankara, Uturuki, Oktoba 27, 2025. (Mustafa Kaya/ kupitia Xinhua)

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kulia) na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer wakionyesha nyaraka za makubaliano zilizosainiwa huko Ankara, Uturuki, Oktoba 27, 2025. (Mustafa Kaya/kupitia Xinhua)

ANKARA – Uturuki imesaini makubaliano jana Jumatatu ya kununua ndege 20 za kivita za Eurofighter Typhoon kutoka Uingereza kwa pauni za Uingereza bilioni 8 (dola za Kimarekani bilioni 10.64), wakati Ankara ikitafuta kuimarisha uwezo wake wa ulinzi katika hali yenye misukusuko ya kikanda.

Kufuatia hafla ya kusaini makubaliano hayo ya miaka 10 mjini Ankara, iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer aliyekuwa ziarani nchini humo, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesifu makubaliano hayo akiyaelezea kuwa ni "ishara mpya ya uhusiano wa kimkakati kati ya washirika wetu wawili wa karibu" na alisema "pia yatafungua mlango wa miradi ya pamoja ya viwanda vya ulinzi wa nchi."

Starmer, kwa upande wake, amesema nchi hizo mbili zinapiga hatua moja mbele kuelekea "uhusiano wa wenzi wa kimkakati ulioimarishwa."

"Kwa hatua ya kwanza ya ushirikiano huu kati ya nchi mbili, Uingereza itaipatia Uturuki ndege 20 za kivita za Eurofighter Typhoon, pamoja na chaguo la kuipatia zaidi katika siku za baadaye," amesema.

Hii ni ziara ya kwanza ya Starmer nchini Uturuki tangu achaguliwe kuwa waziri mkuu wa Uingereza mwezi Julai 2024. Wakati wa ziara yake hiyo, viongozi hao wawili walifanya mazungumzo ya ana kwa ana katika Ikulu ya Rais mjini Ankara, ikifuatiwa na mikutano kati ya wajumbe.

Mapema ya siku hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Yasar Guler aliwaambia waandishi wa habari kwamba nchi hiyo inapanga kununua ndege za kivita 44 za Eurofighter Typhoon kwa jumla -- ndege 12 kutoka Qatar, 12 kutoka Oman, na 20 kutoka Uingereza, na makabidhiano ya ndege yanakadiriwa kuanzia mwanzoni mwa mwaka ujao.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha