Wataalamu wa China na Afrika waunganisha nguvu kusukuma mbele ushirikiano juu ya usalama wa chakula na kilimo cha kisasa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 28, 2025

ADDIS ABABA - Mkutano Mkuu wa 2025 wa Muungano wa China na Afrika wa Uvumbuzi wa Sayansi na Teknolojia ya Kilimo (CAASTIA) umeanza rasmi jana Jumatatu mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, ukilenga ushirikiano kwa ajili ya usalama wa chakula na maendeleo ya kilimo cha kisasa barani Afrika.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa Akademia ya Sayansi ya Afrika Lise Korsten amesema safari ya China katika maendeleo ya kilimo ya China, ilijidhihirisha kwa kilimo cha mazao mengi, minyororo ya thamani iliyoendelezwa, na mafanikio mapya katika kilimo cha kidijitali, ikitoa uzoefu muhimu kwa Afrika.

Kwa mujibu wa mkuu huyo, China inaonyesha mfano mzuri katika kilimo chenye mavuno mengi, kinachochochewa na teknolojia, ikilisha karibu asilimia 20 ya idadi ya watu duniani kwa kutumia chini ya asilimia 9 ya ardhi inayofaa kilimo duniani. Wakati huo huo, Afrika inakabiliwa na ukosefu wa chakula licha ya kuwa na asilimia 60 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani.

"Kitendawili hiki cha ardhi na watu kinasisitiza hitaji la ushirikiano wenye usawa: Ushirikiano unaooanisha uwezo bora wa Afrika ambao haujatumika na uvumbuzi uliothibitishwa wa China ili kujenga mfumo himilivu wa chakula duniani," amesema Korsten.

Jiang Feng, mkuu wa Tume ya China katika Umoja wa Afrika (AU), amesema China iko tayari kuchangia uzoefu wake katika maendeleo ya kilimo na kushirikiana kupunguza umaskini vijijini na nchi za Afrika ili kufikia maendeleo ya pamoja.

Amesisitiza kwamba mapinduzi ya sasa ya kiteknolojia ya kilimo, yanayochochewa na bioteknolojia, teknolojia ya kidijitali, na vifaa vya AI, yanatoa fursa mpya kwa China na Afrika kuboresha tija ya kilimo na kuimarisha mwitikio wao kwa changamoto duniani.

Gaspard Banyankimbona, kamishna wa elimu, sayansi, teknolojia na uvumbuzi wa AU, amesema China na Afrika zinaweza kushirikiana kuendeleza mazao yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi, mifumo endelevu ya usimamizi wa udongo na maji, zana za tahadhari za mapema kuhusu wadudu na hali mbaya ya hewa, na jukwaa la kidijitali ambalo linawezesha wakulima wadogo barani Afrika.

Mkutano huo wa siku tatu, unaondaliwa kwa pamoja na Akademia ya Sayansi ya Kilimo ya China, Akademia ya Sayansi ya Afrika, na Tume ya China katika AU, unawaleta pamoja wanasayansi, watunga sera, na wawakilishi zaidi ya 200 kutoka taasisi za kilimo kote China na Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha