Lugha Nyingine
Mashindano ya upishi yaonyesha kuongezeka kwa kina mawasiliano ya kitamaduni kati ya China na Kenya
![]()  | 
| Mtembeleaji akipiga picha za chakula cha Kichina kwenye Mashindano ya Afrika ya Ubingwa wa Vyakula vya Kichina 2025 yaliyofanyika Nairobi, Kenya, Oktoba 30, 2025. (Xinhua/Li Yahui) | 
NAIROBI - Mashindano ya Afrika ya Ubingwa wa Vyakula vya Kichina 2025, ya kwanza ya aina yake kufanyika barani Afrika, yamefanyika Alhamisi wiki hii katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, yakionyesha kuongezeka kwa kina kwa mawasiliano ya kitamaduni kati ya China na Kenya.
Maafisa waandamizi wa serikali, wanadiplomasia, na watendaji wa sekta husika walihudhuria mashindano hayo, ambapo wapishi kutoka China, nchi kadhaa za Afrika, Marekani, na Australia walionyesha ujuzi wao katika kupika vyakula vya Kichina.
John Ololtuaa, katibu mkuu wa Idara ya Mambo ya Utalii katika Wizara ya Utalii na Wanyamapori ya Kenya, amesema mashindano hayo yanasisitiza kuchangamana kwa tamaduni za China na Afrika na uhusiano mkubwa wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili.
"Mashindano haya ya leo yanatoa fursa kubwa zaidi ya kuonyesha upishi wa Kichina kwa dunia," amesema Ololtuaa, akiongeza kuwa anatarajia kuona na kula vyakula vya Kichina vilivyochanganywa na ladha za Kenya.
Balozi wa China nchini Kenya Guo Haiyan ameelezea historia ya kujitokeza kwa ladha mbalimbali za vyakula vya Kichina barani Afrika kuwa ni simulizi dhahiri ya mawasiliano na mwingiliano wa tamaduni.
"Katika jukwaa la leo, niamini kwamba tutaona upishi wenye ustadi wa vyakula vya kijadi vya Kichina vilevile michangamano ya kibunifu na viungo vya Kiafrika. Hii inawakilisha kiini cha falsafa ya upishi ya Kichina – mapatano katika uanuwai, na inaonyesha moyo wa urafiki kati ya China na Afrika – uzuri katika kuthaminiana," amesema Guo.
Mark Ogendi, mkuu na afisa mtendaji mkuu wa Chuo cha Utalii cha Kenya, amesifu mashindano hayo ya vyakula kwa kutoa jukwaa la kuongeza mawasiliano ya kuvuka tamaduni mbalimbali kati ya taasisi za ndani ya Kenya na zile za China.
Yakiwa ni sehemu ya Msimu wa Utamaduni na Utalii wa China na Kenya 2025, mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku nzima yaliandaliwa kwa pamoja na Shirikisho la Upishi wa Kichina Duniani, Jumuiya ya Vyakula na Utamaduni wa China ya Kenya, na Chuo cha Utalii cha Kenya, taasisi kuu ya mafunzo ya ukarimu na utalii ya nchi hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




