Lugha Nyingine
Mashambulizi mapya ya anga ya Israeli yaikumba Kusini mwa Lebanon, yakipima makubaliano dhaifu ya kusimamisha vita (6)
![]() |
| Picha iliyopigwa Novemba 6, 2025 ikionyesha watu wakikagua majengo yaliyobomolewa na mashambulizi ya anga ya Israeli katika mji wa kusini wa Tayr Debba, Lebanon. (Picha na Ali Hashisho/Xinhua) |
BEIRUT/JERUSALEM - Israeli imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga kusini mwa Lebanon jana Alhamisi, na kuwaonya wakazi wa vijiji kadhaa kuhama huku, mvutano ukiendelea kuongezeka licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusimamisha mapigano ya karibu mwaka mmoja ambapo wachambuzi wanaamini kwamba kuongezeka huko kwa mapigano ni sehemu ya mkakati wa Israeli wa kuishinikiza Hezbollah kwa makusudi.
Jeshi la Israeli limesema jana Alhamisi katika taarifa kwamba "limeanza mfululizo wa mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Hezbollah kusini mwa Lebanon," huku msemaji wa jeshi hilo Avichay Adraee akitoa onyo maalum ya kuhamishwa kwa wakazi wa vijiji vya Al-Tayyiba, Tayr Debba, na Aita al-Jabal.
Vyanzo vya habari vya Lebanon vimesema mashambulizi hayo ya anga ya Israeli yameua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine wanane katika manispaa ya Toura kusini mwa nchi hiyo, na kumjeruhi mtu mmoja mwingine huko Tayr Debba.
Mashambulizi hayo mapya yamesababisha watu kuhama makazi yao, huku foleni kubwa ya magari ikiripotiwa wakati wakazi wakikimbia maeneo yaliyolengwa. Shule kadhaa za binafsi katika eneo la Nabatieh, kusini mwa Lebanon zimetangaza kufungwa leo Ijumaa ili kuepuka kuwaweka wanafunzi na walimu hatarini.
Mashambulizi hayo ni mapya katika mfululizo wa operesheni za Israeli zinazozidi kuongezeka, ambazo vyanzo vya habari vya Lebanon vimesema zimeongezeka tangu mapema Novemba.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, jeshi la Israeli lilifanya operesheni 22 za kijeshi katika wiki ya kwanza ya Novemba pekee, zikiwemo mashambulizi ya anga, mashambulizi ya mizinga, na ubomoaji wa nyumba.
"Operesheni hizi za kijeshi zimesababisha vifo vya watu wanane na wengine 10 kujeruhiwa, uharibifu wa nyumba sita, uchomaji wa matingatinga manne, na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ya kiraia," vyanzo hivyo vya habari vimeliambia Shirika la Habari la China, Xinhua jana Alhamisi.
Hiyo inafuatia matukio ya Oktoba, ambapo Wizara ya Afya ya Lebanon iliripoti vifo vya watu 28 na wengine 54 kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Israel.
Pia siku hiyo ya Alhamisi, chanzo kikuu cha idara ya ujasusi ya jeshi la Lebanon kimesema kwamba "Jeshi la Lebanon linafanya kazi kwa nguvu zote kusafisha maeneo kusini mwa Mto Litani ili kuondoa silaha na wapiganaji," likiwa limeanzisha ngome katika maeneo 118 na kuharibu maeneokadhaa ya kijeshi pamoja na mahandaki nyingi.
Wakati huo huo, Hezbollah imetoa barua ya wazi jana Alhamisi kwa Rais wa Lebanon Joseph Aoun, Spika wa Bunge Nabih Berri, na Waziri Mkuu Nawaf Salam, ikionya dhidi ya "kuingia kwenye mitego ya mazungumzo" na Israeli.
"Hakuna maslahi ya taifa katika mazungumzo ya kisiasa na adui Israeli," taarifa hiyo inasema, ikiongeza kuwa Israeli inatumia "vitishio na udanganyifu" kulazimisha masharti, yakiwemo ya kulemewa kwa silaha za Hezbollah, kama sharti la kukomesha uhasama, jambo ambalo "halikubaliki na halimo katika azimio la makubaliano ya kusimamisha mapigano."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




