Lugha Nyingine
Ramaphosa atarajia mkutano wa G20 kuhimiza mageuzi ya fedha ya kimataifa, kushughulikia ukosefu wa usawa duniani (6)
![]() |
| Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akizungumza kwenye kikao cha maswali na majibu katika Bunge la Taifa la Afrika Kusini mjini Cape Town, Afrika Kusini, Novemba 6, 2025. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua) |
CAPE TOWN - Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kwamba Mkutano ujao wa Viongozi wa Kundi la nchi 20 (G20) unatarajiwa kuchukua hatua madhubuti za kuufanyia mgeuzi mfumo wa kifedha wa kimataifa wakati huohuo ukishughulikia pengo linalozidi kuongezeka la utajiri na mapato duniani. Akizungumza jana Alhamisi kwenye kikao cha maswali na majibu katika Bunge la Taifa mjini Cape Town, Rais Ramaphosa amesema uenyekiti wa zamu wa G20 wa Afrika Kusini unalenga "kujenga mfumo wa fedha wa kimataifa ulio thabiti zaidi, wenye ufanisi zaidi na himilivu zaidi."
Amesema kuwa moja ya matokeo makubwa yanayotarajiwa kutoka kwenye mkutano huo wa viongozi, uliopangwa kufanyika Johannesburg baadaye mwezi huu, ni "makubaliano juu ya kuimarisha benki za maendeleo za kimataifa, kama vile Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, na Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB."
Amefafanua kwamba hatua hiyo itajenga juu ya kazi iliyofanwa na uenyekiti wa zamu wa G20 wa Brazil ili kuzifanya taasisi hizo ziwe na ufanisi zaidi katika kusaidia nchi kufikia malengo yao ya maendeleo endelevu.
"Tunatarajia mkutano huo wa viongozi kutoa ahadi ya kisiasa kushughulikia changamoto za madeni katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati. changamoto hizi za madeni zinapunguza nafasi yao ya kifedha, uwezo wao wa kukabiliana na umaskini na hali ya ukosefu wa usawa, pamoja na uwezo wao wa kuwekeza katika ukuaji na maendeleo." Ramaphosa amesema.
Ameongeza kuwa Azimio la Viongozi la Johannesburg linatarajiwa kujumuisha "ahadi ya kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Mfumokazi wa Pamoja wa G20 wa Kushguhulikia Madeni kwa namna inayoweza kutabirika, kwa wakati na iliyoratibiwa."
Rais huyo amesema, mkutano huo wa viongozi utahimiza jumuiya ya kimataifa kuunga mkono nchi zilizo hatarini kwa ajenda imara ya mageuzi ambazo madeni yao ni endelevu lakini zinakabiliwa na changamoto za ukwasi.
Amesema katika kushughulikia suala la ukosefu wa usawa, Kamati Maalum ya Wataalamu Huru wa G20 kuhusu Ukosefu wa Usawa wa Utajiri Duniani, inayoongozwa na mshindi wa Tuzo ya Nobel Joseph Stiglitz, tayari imewasilisha ripoti muhimu wiki hii.
"Kamati hiyo imetoa uchambuzi wa kina kuhusu ukosefu wa usawa duniani na kupendekeza hatua mahsusi ambazo viongozi wanapaswa kuchukua ili kukabiliana na changamoto hii," Ramaphosa amesema.
Ameongeza kuwa hatua hizo zinajumuisha kuzifanyia mageuzi kanuni za uchumi wa kimataifa, kutoza kodi kwa haki kwa mashirika ya kimataifa, na watu wenye utajiri mkubwa, na kuanzisha "jopo jipya la kimataifa na huru litakalofuatilia mwelekeo wa ukosefu wa usawa na kuhakikisha sera za kukabiliana na hali hiyo."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




