Lugha Nyingine
Ufunguzi wa Michezo ya Kitaifa ya China waonesha umoja, utamaduni na uvumbuzi (2)
![]() |
| Picha iliyopigwa Novemba 9, 2025 ikionyesha mwonekano wa jumla wa sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya 15 ya Kitaifa ya China mjini Guangzhou, Mkoani Guangdong, kusini mwa China. (Xinhua/Li Xin) |
GUANGZHOU - Michezo ya 15 ya Kitaifa ya China, inayofanyika kwa mara ya kwanza katika Guangdong, Hong Kong na Macao, imefunguliwa rasmi jana Jumapili jioni huku sherehe ya ufunguzi wake ikionyesha urithi wa kitamaduni na uvumbuzi wa kiteknolojia.
Michezo ya Kitaifa yafanyika mikoa mitatu
Kwa mara ya kwanza tangu Michezo ya mwanzo ya Kitaifa ya China ifanyike mwaka 1959, michezo hiyo inafanyika katika mikoa mitatu kwa wakati mmoja: Guangdong, Hong Kong na Macao.
Sherehe ya ufunguzi imesisitiza umoja, huku wanamichezo kutoka mikoa yote hiyo mitatu wakiingia uwanjani pamoja na kupokelewa kwa makofi mengi ya shangwe. Bendera za taifa za China katika uwanja mkuu mjini Guangzhou, vilevile Hong Kong na Macao, zilipandishwa kwa wakati mmoja, ikionyesha ushirikiano wa Eneo la Ghuba Kuu na fahari ya taifa.
Ndoto ya pamoja yawashwa
Wanamichezo mahiri kutoka maeneo mbalimbali ya China walibeba mwenge, uliochukuliwa kutoka kina cha mita 1,522 ya Bahari ya Kusini ya China, na kuleta kwenye uwanja huo.
Wabeba mwenge wa mwisho, mwanamichezo wa Guangdong Su Bingtian, ambaye ni mshikiliaji rekodi ya Asia ya mita 100, bingwa wa Olimpiki wa mchezo wa fencing wa Hong Kong Cheung Ka Long, na mwanamchezo wa Macao Li Yi, mshindi wa medali ya dhahabu ya wushu ya Michezo ya Asia, waliwasha mwenge mkuu wa michezo hiyo.
Duara na maji yawakilisha umoja
Kaulimbiu ya umoja ilionyeshwa kwenye jukwaa kuu la mviringo lililozungukwa na jukwaa la maji lenye umbo la pete.
"Tulitumia umbo la duara kama kipengele kikuu, huku jukwaa la mviringo na mapambo yake mbalimbali yakielezea ndoto ya kuungana," amesema Huang Peiling, naibu mkurugenzi wa sherehe hiyo ya ufunguzi.
Urithi wa kitamaduni waoneshwa
Maonyesho yameonyesha tamaduni za Eneo la Ghuba Kuu pamoja na mambo mapya, yakiwemo ngoma ya Yingge, ngoma ya simba ya Guangdong na opera ya Canton.
Sherehe hiyo pia imetoa heshima kwa urithi wa sanaa ya wushu ya eneo hilo, ikiwataja watu maarufu kama vile Wong Fei Hung, Ip Man na Bruce Lee, na kuweka majina hayo maarufu pamoja na michezo ya kisasa.
Teknolojia yachochea uvumbuzi
Likiwa moja ya maeneo yenye uhai zaidi ya kiuchumi ya China, Eneo la Ghuba Kuu limetoa kipaumbele mada za kiteknolojia kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi.
Kwa kutumia akili mnemba, AR, VR na roboti, timu ya uzalishaji maudhui ya sherehe hiyo imewasilisha dhana ya "kuleta bahari kwenye ukumbi." Kwenye jukwaa la ukubwa wa mita 5,000 za mraba, teknolojia iliwezesha wanaofanya maonyesho zaidi ya 3,000 kuunda taswira iliyoonekana kama maelfu ya watu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




