Lugha Nyingine
Mradi wa kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo uliojengwa na Kampuni ya China wawezesha wenyeji, kuboresha maisha nchini Afrika Kusini
![]() |
| Picha hii iliyopigwa Oktoba 22, 2025 ikionyesha mitambo ya upepo ya Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Upepo wa De Aar huko De Aar, Northern Cape, Afrika Kusini.(Xinhua/Han Xu) |
CAPE TOWN - Katika alasiri yenye upepo kwenye nyanda kame za Jimbo la Northern Cape la Afrika Kusini, Xolani Taute mwenye umri wa miaka 31 alisimama chini ya mitambo mirefu myeupe ya kuzalisha umeme kwa upepo, ambayo mapanga yake yakikata anga ya buluu juu ya mji mdogo wa De Aar.
Awali alikuwa fundi umeme asiye na ajira na hakuwa na matarajio ya kusoma zaidi au kupata kazi ya uhakika. Kwa sasa Taute ni fundi mwanagenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa upepo -- ushuhuda wa jinsi nishati mbadala inavyobadilisha maisha ya wenyeji.
"Longyuan imebadilisha maisha yangu kwa njia nyingi. Ninajivunia sana kile ambacho Longyuan imefanya hapa De Aar." Taute ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua, macho yake yaking'aa kwa msisimko.
Miaka minne iliyopita, Taute alikuwa akihangaika kupata kazi hadi alipojua kuwa Kampuni ya Nishati Mbadala ya Longyuan Tawi la Afrika Kusini (Longyuan SA), tawi linalomilikiwa kabisa na Kampuni ya Nishati ya Longyuan ya Kundi la Kampuni za Uwekezaji wa Nishati la China (CHN Energy), ilikuwa ikitafuta wafanyakazi kwa ajili ya Mradi wake wa Kuzalisha Umeme kwa Upepo wa De Aar. Alitoa maombi yake na, kwa mshangao wake, alipewa si tu kazi bali mustakabali wa maisha yake.
Longyuan SA ilifadhili mafunzo yake katika chuo cha ufundi mjini Cape Town. Baadaye alipata mafunzo ya vitendo katika shamba la upepo la De Aar kabla ya kujiunga na kampuni hiyo mwaka 2023 akiwa fundi mwanagenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa upepo.
"Walilipia masomo yangu ya chuo na malazi yangu, gharama ya usafiri, chakula, kila kitu," Taute amekumbuka.
Kwake, faida kubwa kwa vijana wenyeji kama yeye si ajira tu bali fursa ya kujifunza na kuwa wabobezi wa teknolojia mpya.
Ukiwa ulikamilishwa mwaka 2017, Mradi huo wa Kuzalisha Umeme kwa Upepo wa De Aar unasimama kama mfano kinara wa ushirikiano kati ya China na Afrika Kusini chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja.
Kwa uwekezaji wa takriban yuan takriban bilioni 2.5 (dola za Kimarekani karibu milioni 352) na uwezo wa kusambaza umeme megawati 244.5, mradi wa kwanza wa kuzalisha umeme kwa upepo barani Afrika ulioendelezwa, kujengwa na kuendeshwa na kampuni ya umeme ya China, ukiibuka kuwa shamba kubwa zaidi la kuzalisha umeme kwa upepo nchini Afrika Kusini.
Mitambo yake 163 ya upepo huzalisha kilowati takriban milioni 770 za umeme safi kwa mwaka, ikitoa umeme kwa nyumba zipatazo 300,000 za Afrika Kusini na kupunguza uhaba wa umeme wa nchi hiyo.
Zaidi ya kutoa nishati ya kijani, kampuni hiyo Longyuan SA imejikita katika "kufundisha watu ujuzi wa kujipatia kipato" -- kukuza vipaji vya wenyeji, kuboresha maisha na kuchochea ukuaji wa kikanda.
Hadi sasa, mradi huo umeshatoa mafunzo kwa mafundi vijana zaidi ya 110, huku asilimia zaidi ya 80 ya wafanyakazi wake sasa ni wenyeji, wengi wao wakiwa na nafasi muhimu za uendeshaji na usimamizi.
"Sasa ninaweza kuwatunza familia yangu, na dada zangu na kaka zangu. Wamebadilisha maisha yangu." amesema Taute.
Longyuan SA pia inaendesha programu ya ufadhili wa masomo yenye thamani ya randi takriban milioni 4.5 (karibu dola za Marekani 263,200) kwa mwaka ili kusaidia wanafunzi kutoka familia zenye kipato cha chini kuendelea na masomo yao. Hadi sasa, wanafunzi 390 wamefaidika, akiwemo Daswin Basson mwenye umri wa miaka 30, ambaye sasa ni fundi mkufunzi wa matengenezo katika Mradi wa De Aar.
Katika mji wenye vituo vichache vya matibabu, wakazi mara nyingi huona basi jeupe la kliniki likifanya mizunguko yake, ambalo ni jitihada nyingine ya Longyuan SA.
Likiwa na vitengo vya meno na macho, basi hilo hutoa huduma za matibabu bila malipo kwa wakazi wapatao 9,000 kila mwaka na limehudumia watu zaidi ya 50,000 tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2020.
Programu za uwajibikaji wa kijamii za kampuni hiyo pia zinajumuisha kufadhili nyumba za wazee wenyeji ili kuhakikisha chakula na huduma kwa wazee maskini, kujenga na kuendesha vituo vya elimu ya awali ya watoto wachanga ili kutoa elimu bure kwa mamia ya watoto kutoka familia zenye kipato cha chini na zenye mahitaji maalum, na kuwekeza mamilioni ya randi kutengeneza miundombinu ya maji ya mji huo, kubadilisha mabomba ya zamani na kusafisha mabwawa ili kupata maji safi ya kunywa kwa wakazi zaidi ya 2,000.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




