Lugha Nyingine
Mkutano wa Tabianchi wa COP30 waanza Belem, Brazil

Washiriki wakiwasili kwenye ukumbi wa mkutano wa 30 wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa mjini Belem, Brazil, Novemba 10, 2025. (Picha/cfp)
BELEM, Brazil - Mkutano wa 30 wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kwa jina la COP30, umefunguliwa rasmi jana Jumatatu mjini Belem, Brazil, kwa lengo la kurejesha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katikati ya vipaumbele vya kimataifa, kwa mujibu wa mamlaka za serikali ya Brazil.
Kwenye hafla ya ufunguzi, Rais wa COP29 Mukhtar Babayev ametoa wito wa kufikia malengo ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi uliofanyika mwaka jana mjini Baku, mji mkuu wa Azerbaijan.
Rais wa COP30 Andre Correa do Lago amemshukuru Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva kwa kumteua na akasisitiza kwamba COP30 lazima itoe suluhisho.
Licha ya changamoto za hivi karibuni, hali ya maisha ya watu katika nchi na maeneo mbalimbali duniani inaweza na lazima iendelee kuboreka, Correa do Lago amesisitiza. "Sayansi, elimu, utamaduni ndiyo njia tunayopaswa kufuata," amesema.
"Ushirikiano wa pande nyingi bila shaka ndiyo njia sahihi ya kusonga mbele katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Mada kadhaa, zikiwemo za uhimilivu wa tabianchi, mabadiliko ya haki, na utekelezaji wa usawa wa kimataifa wa Mkataba wa Paris, zinatarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano huo.
Wajumbe wa nchi na maeneo zaidi ya 190 wamejiandikisha kushiriki kwenye mkutano huo, ambao umepangwa kuendelea hadi Novemba 21, kwa mujibu wa rais huyo wa COP30.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



