Biashara ya EAC yapanda hadi dola bilioni 38.2 katika robo ya pili huku mauzo ya nje yakipanda kwa asilimia 40

(CRI Online) Novemba 11, 2025

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imerekodi ukuaji mkubwa katika biashara ya bidhaa ya kimataifa kwenye robo ya pili ya 2025, ikionesha uhimilivu wa kiuchumi na uwezo wa kiushindani unaokua wa kanda hiyo katika masoko ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Takwimu za Robo Mwaka za EAC zilizotolewa Jumatatu, jumla ya biashara kwa jumuiya hiyo yenye nchi wanachama wanane iliongezeka kwa asilimia 28.4 hadi kufikia dola bilioni 38.2 za Marekani, ikiwa ni kuongezeka kutoka dola bilioni 29.7 katika robo hiyo hiyo mwaka jana.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa, ukuaji huo ulichochewa zaidi na mauzo ya nje, ambayo yaliongezeka kwa asilimia 40.5 hadi kufikia dola bilioni 18.6 za Marekani huku kukiwa na ongezeko la mahitaji ya kimataifa ya bidhaa za Afrika Mashariki.

Kulingana na takwimu hizo, biashara na mataifa mengine ya Afrika iliongezeka kwa kiasi kikubwa kwa asilimia 42.9 hadi kufikia dola bilioni 9.3, ikichukua karibu robo ya biashara yote ya kanda hiyo, huku biashara ya ndani ya EAC ikiongezeka kwa asilimia 24.5 hadi kufikia dola bilioni 4.6, ikiwakilisha asilimia 12.1 ya jumla ya biashara ya jumuiya hiyo.

Taarifa hiyo ya EAC imesema, kuongezeka kwa uhusiano na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kumechangia asilimia 9.9 na asilimia 15.2 mtawalia, katika biashara ya kanda hiyo.

Imesema China, Falme za Kiarabu, Afrika Kusini, na Singapore ziliendelea kuwa maeneo bora zaidi ya mauzo ya nje ya EAC, huku China ikiendelea kuwa chanzo kikuu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha