Lugha Nyingine
Barabara Kuu iliyojengwa kwa msaada wa China yafunguliwa rasmi nchini Namibia, ikiimarisha muunganisho wa kikanda

Veikko Nekundi (kushoto), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Namibia, na Zhao Weiping, Balozi wa China nchini Namibia, wakihudhuria hafla ya kukata utepe kwa ajili ya ufunguzi wa Barabara Kuu ya Dkt. Hage G. Geingob iliyojengwa kwa msaada wa China mjini Windhoek, Namibia, Novemba 10, 2025. (Xinhua/Lin Jing)
WINDHOEK - Namibia imezindua rasmi Barabara Kuu ya Dkt. Hage G. Geingob jana Jumatatu katika mji mkuu, Windhoek, ikishuhudia kukamilika kwa mradi kinara wa miundombinu unaotarajiwa kubadilisha usafirishaji wa kikanda na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi.
Serikali ya Namibia ilifadhili awamu ya kwanza na ya pili ya mradi huo mwaka 2016 na 2020, huku Kampuni ya China ya Uhandisi ya Zhong Mei ikijenga awamu ya tatu mwaka 2021, likisaidiwa na ruzuku ya serikali ya China ya yuan milioni 447 (dola za Kimarekani karibu milioni 62.8).
Mradi huo uliojengwa kwa msaada wa China, barabara hiyo ya kilomita 21.3 yenye njia nne za pande zote mbili inayojulikana kuwa Awamu ya 2B ya mpango wenye awamu tatu, umekabidhiwa rasmi kufuatia kusainiwa kwa vyeti vya kukamilika.
Kufuatia kufunguliwa kwa barabara kuu hiyo mpya, muda wa kusafiri kati ya eneo la katikati mwa Jiji la Windhoek na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hosea Kutako umepunguzwa kutoka dakika takriban 50 hadi dakika zaidi ya 20 tu, ikiboresha kwa kiasi kikubwa ufanisi wa usafirishaji na kupunguza msongamano katika mji mkuu.
Kwenye hotuba yake kuu, Waziri wa Ujenzi na Usafirishaji wa Namibia Veikko Nekundi amepongeza mradi huo kama hatua muhimu katika maendeleo ya kitaifa ya Namibia na kuinua jamii.
"Barabara Kuu hii ni njia muhimu inayounganisha mji mkuu wetu na lango kuu la taifa letu, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hosea Kutako, na inaboresha ufikaji kwenye vituo vya kimkakati kama vile Bandari ya Ghuba ya Walvis," amesema, akiongeza kuwa mradi huo ni sehemu muhimu ya mpango wa maendeleo ya njia kuu za kikanda za Namibia, na ikihimiza biashara kati ya kanda mbalimbali.
Nekundi amesisitiza kwamba barabara hiyo inasimama kama ushuhuda kwa dhamira ya Namibia ya kuhakikisha usalama katika mtandao wake wa barabara wa kitaifa na kusisitiza umuhimu wa kudumisha ushirikiano ulio na uwiano kati ya miradi ya kimataifa na ya ndani.
Wakati wa ujenzi, mradi huo uliajiri Wanamibia takriban 850 na kuhusisha wakandarasi wadogo 54 wa ndani, ukitoa mchango katika ukuzaji wa ujuzi na utoaji wa ajira.
Conrad Lutombi, afisa mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Barabara ya Namibia, ambayo inasimamia mtandao wa barabara wa kitaifa wa Namibia, ameipongeza China kwa kuendelea kutoa msaada wake.
"Inaonyesha dhamira ya China kwa mabadiliko ya miundombinu ya Afrika na kwa kweli, inaonyesha urafiki wa hali zote." amesema.
Balozi wa China nchini Namibia Zhao Weiping ameieleza barabara kuu hiyo kuwa ni "ushuhuda dhahiri wa urafiki kati ya China na Namibia."
"Barabara hii pana na laini si tu kwamba inabeba matarajio ya watu wa Namibia kwa maisha bora lakini pia inaondoa vikwazo katika kiungo muhimu kwa muunganisho wa miundombinu ya kikanda, ikiweka msingi imara kwa ajili ya ujenzi wa njia za usafirishaji wa Jangwa la Kalahari wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika," amesema.
Maafisa hao pia wamesema kuwa barabara kuu hiyo mpya ni sehemu ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, mfumokazi wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, na Mpango wa Ustawi wa Harambee wa Namibia.

Gari likipita chini ya daraja lenye bango lenye maandishi "Msaada wa China" kwenye Barabara Kuu ya Dkt. Hage G. Geingob iliyojengwa kwa msaada wa China karibu na Windhoek, mji mkuu wa Namibia, Novemba 10, 2025. (Xinhua/Lin Jing)

Picha iliyopigwa Mei 25, 2025 ikionyesha Barabara Kuu ya Dkt. Hage G. Geingob iliyojengwa kwa msaada wa China nchini Namibia. (Kundi la Kampuni za China za Uhandisi la Zhong Mei/kupitia Xinhua)

Veikko Nekundi, Waziri wa Ujenzi na Usafirishaji wa Namibia, akitoa hotuba kwenye hafla ya uzinduzi wa Barabara Kuu ya Dkt. Hage G. Geingob iliyojengwa kwa msaada wa China mjini Windhoek, Namibia, Novemba 10, 2025. (Xinhua/Lin Jing)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



