Lugha Nyingine
EAC yazindua mpango wa majaribio wa malipo ya papo hapo kati ya Tanzania na Rwanda
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeanza kutekeleza mpango tangulizi ili kuunda mtandao wa malipo ya papo hapo ya kikanda, utakaoanza na mradi wa majaribio unaounganisha mifumo ya taifa ya malipo ya rejareja ya papo hapo ya Tanzania na Rwanda.
Taarifa iliyotolewa na EAC jana Jumanne imesema kuwa mradi huo, ambao kwa sasa unafanyiwa kazi kiufundi kwenye mkutano wa ngazi ya juu mjini Kigali, nchini Rwanda, utaunganisha mfumo wa malipo ya kitaifa wa Tanzania na ule wa swichi ya malipo ya kitaifa ya kidijitali ya Rwanda, RSwitch.
Taarifa hiyo ya EAC imesema kuwa, mara tu mradi huo utakapoanza kufanya kazi, utawezesha miamala ya mara moja na yenye gharama nafuu kati ya akaunti za benki na waleti za simu katika nchi hizo mbili.
Afisa mkuu wa teknolojia ya habari wa EAC Daniel Murenzi amesema kuwa kazi hiyo ya maandalizi inaashiria hatua muhimu katika ajenda ya mafungamano ya malipo ya kikanda, ikiisogeza jumuiya hiyo karibu zaidi na kukamilisha mfumo mmoja wa malipo ya papo hapo wa EAC.
Taarifa hiyo imesema kwamba muunganisho wa Tanzania na Rwanda unatumika kama msingi wa jaribio la uthibitisho wa dhana kwa ajili ya kuonyesha uwezekano wa kiufundi na kiutendaji wa kuunganisha mifumo ya malipo katika kanda nzima. Aidha, imeongeza kuwa mpango huo utatumika kama mfano wa upanuzi kwa nchi zote wanachama wa EAC.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



