Lugha Nyingine
AU, UN zajadili ushirikiano na hatua za pamoja juu ya amani, usalama na maendeleo
Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) zimejadili utekelezaji wa mifumo ya ushirikiano kati ya mashirika hayo mawili vilevile hatua za pamoja na changamoto zinazohusiana na amani, usalama, maendeleo na haki za binadamu katika mkutano wao wa tisa wa mwaka kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York jana Jumatano.
Majadiliano hayo ya ngazi ya juu, yaliyoongozwa kwa pamoja na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Mahmoud Ali Youssouf na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, pia yamegusia mada kama vile ufadhili wa maendeleo, hatua za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na utekelezaji wa agenda ya mkakati wa Afrika kwa wanawake, amani na usalama.
Akitoa wito wa kuufanyia mageuzi usanifu wa mambo ya fedha wa kimataifa ili uweze kuakisi dunia ya leo na kuhudumia vizuri mahitaji ya nchi zinazoendelea, haswa barani Afrika, Guterres amesema kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya mkutano huo kwamba, lazima uwe "jumuishi, wakilishi, wenye usawa na fanisi zaidi."
Katika maelezo yake, Youssouf amesema mkutano huo wa mwaka wa AU na UN ni jukwaa la kimkakati la mashauriano na uratibu wa mara kwa mara kati ya mashirika hayo mawili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



