Lugha Nyingine
Afrika Kusini yaweka lengo jipya la mfumuko wa bei katika asilimia 3
CAPE TOWN - Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini Enoch Godongwana ametangaza lengo jipya la mfumuko wa bei la asilimia 3, likiwa na kiwango cha uhimilivu cha asilimia 1, ambapo wakati akitoa Taarifa ya Sera ya Bajeti ya Muda wa Kati Bungeni jana Jumatano, Godongwana amesema kiwango hicho cha uhimilivu kinatoa unyumbulifu wa kukabiliana na mishtuko yoyote isiyotarajiwa ya mfumuko wa bei.
"Uamuzi huu unafuatia makubaliano kati ya Gavana wa Benki Kuu ya Afrika Kusini, mashauriano yangu na Rais, pamoja na Baraza la Mawaziri. Lengo hili jipya linachukua nafasi mara moja ya lengo la awali la kati ya asilimia 3 na 6 na litatekelezwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo," waziri huyo amesema.
Godongwana amesema gharama za kibajeti za muda mfupi za lengo hilo la chini -- ambazo ni pamoja na ukuaji mdogo wa pato la ndani la chini (GDP) na mapato -- zitafanya kuwa changamoto zaidi kufikia malengo ya kibajeti.
"Hata hivyo faida za muda mrefu za kuchukua hatua hii zinazidi gharama hizo. Tunaendelea kujitolea kuhakikisha kwamba sera zetu za uchumi wa jumla zinahudumia maslahi bora ya Waafrika Kusini wote," amesema.
Godongwana amesema serikali ya Afrika Kusini pia iko katika njia sahihi ya kudhibiti deni la taifa. "Deni la serikali litadhibitiwa mwaka wa fedha wa 2025 hadi 2026, katika kiwango cha asilimia 77.9 ya Pato la Taifa. Hii ni mara ya kwanza tangu msukosuko wa kifedha wa mwaka 2008 ambapo deni la umma halitakua sawa na asilimia ya Pato la Taifa," amesema.
Wakati huo huo, waziri huyo amesisitiza kuwa matarajio ya kiuchumi ya Afrika Kusini pia yanaathiriwa na maendeleo ya uchumi duniani, huku athari zilizocheleweshwa za ushuru wa upande mmoja uliowekwa na Marekani, pamoja na kuongezeka kujihami kibiashara, vikisababisha hatari za siku za baadaye kwa tija na utulivu wa bei duniani.
"Ndani ya nchi, tunakadiria ukuaji halisi wa Pato la Taifa wa asilimia 1.2 kwa mwaka 2025, zaidi ya mara mbili ya ukuaji wa uchumi wa mwaka 2024," amesema Godongwana, akiongeza kuwa ukuaji halisi wa Pato la Taifa unatarajiwa kuwa wastani wa asilimia 1.8 kati ya mwaka 2026 na 2028.
Kwa mujibu wa Godongwana, mageuzi ya kimuundo ambayo Afrika Kusini imeanza kuyatekeleza, hasa katika sekta za nishati na usafirishaji wa mizigo, yatakuwa muhimu katika kuinua kiwango chake cha ukuaji wa uchumi kufikia viwango vinavyohitajika kwa maendeleo ya nchi.
Ameongeza kuwa mkakati wa nchi hiyo kwa ukuaji wa haraka na hali bora ya fedha unaendelea kuongozwa na nguzo nne, ikiwemo kudumisha utulivu wa uchumi wa jumla, kutekeleza mageuzi ya kimuundo, kujenga uwezo wa serikali, na kusaidia maendeleo ya miundombinu inayochochea ukuaji.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



